SHIRIKA LA NYUMBA JUU !!!: Chakarikeni wajomba, toa nyumba kuukuu,Mijini shida ya nyumba, ipo toka wajukuu

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

HIVI karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu amewaeleza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, shirika hilo limeboresha Mpango Mkakati wake ili uweze kukidhi matarajio ya Serikali na nchi kwa ujumla.

Mchechu ameyabainisha hayo wakati akielezea mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa shirika hilo katika semina ya wabunge iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Msekwa, bungeni jijini Dodoma.

Amesema, shirika limeboresha muundo wa utendaji wake ili uweze kubeba majukumu yaliyoainishwa kwenye Mpango Mkakati na pia limeboresha sera mbalimbali ikiwemo ile ya ubia ambayo inalenga kuongeza ufanisi.

Pia shirika lipo katika mkakati wa kukamilisha miradi mitatu ya nyumba iliyokwama kwa miaka minne katika Jiji la Dar es Salaam ukiwemo ule wa Kawe 711, Morocco Square na GPR.

Katika hatua nyingine, aliweka wazi kuwa,wanatarajia kujenga nyumba mpya 500 katika eneo la Kawe, kuongeza nyumba za makazi na kipaumbele kikiwa katika Jiji la Dodoma huku wakitarajia kukamilisha majengo ya kudumu ya wizara nane za Serikali katika Mji wa Mtumba.

Aidha, mbali na pongezi kwa shirika hilo kupitia utekelezaji miradi mbalimbali ya ujenzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Dkt.Sophia Kongela anasema, ni shauku yao kuona miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo ikiwemo ya ujenzi wa nyumba jijini Dodoma inakamilika kabla ya muda ili kutoa nafasi katika utekelezaji wa miradi mingine nchini.

Dkt.Kongela ameyasema hayo Mei 19,2022 baada ya Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutembelea na kukagua mradi wa nyumba unaojengwa na shirika hilo jijini Dodoma, ambapo imesisitiza ujenzi wa nyumba hizo ufanyike kwa ubora, kiwango na muda uliopangwa kusudi ulete tija kwa nchi.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kwa kuthamini na kutambua kazi nzuri inayofanywa na shirika hilo la umma, ametumia kalamu yake kuandaa shairi maalum ambalo mbali na kupongeza pia linatoa ushauri ambao unalenga kuongeza ufanisi ili shirika liweze kustawi kwa kasi, hatua kwa hatua ungana naye kupitia shairi hapa chini. Karibu...

1:Shirika letu la nyumba, linayo kubwa shauku,
Kasi ya kujenga nyumba, inakua kila siku,
Watu wakalie nyumba, wamalize dukuduku,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

2:Vitu vyakuzingatia, bila ya mtu kushuku,
Ubora kuzingatia, kama muziki wa zuku,
Kwa kasi kumalizia, kuchelewa marufuku,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

3:Tija kubwa yatafutwa, kazi za siku kwa siku,
Uhaba uweze futwa, wakae wapike kuku,
Na huduma wakifwatwa, pia umeme wa luku,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

4:Miradi kule Dodoma, kwenye makao makuu,
Kasi ujenzi ni njema, wameshasema wakuu,
Dasalama na Musoma, pia kasi iwe kuu,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

5:Kwa sasa mwendo mdundo, kasi kama sikukuu,
Mbao mabati na nondo, usambazaji ni juu,
Huko hakuna uvundo, wasimamia wakuu,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

6:Mijini shida ya nyumba, ipo toka wajukuu,
Watu wengi toka shamba, watoto na vitukuu,
Wote wanataka nyumba, makao yao makuu,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

7:Nyie Shirika la Nyumba, twawaona mko juu,
Mambo yenu yanabamba, mnazidi paa juu,
Chakarikeni wajomba, toa nyumba kuukuu,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

8:Alfu na mia tatu, nyumba makao makuu,
Ni nyumba zinajengwa tu, waje wakae wakuu,
Shirika la Nyumba letu, kipato kipande juu,
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

9:Ni Iyumbu na Chamwino, huku makao makuu,
Mandhari sasa ni nono, Dodoma yapaa juu,
Ni mwema mshikamano, Shirika la Nyumba juu!
NHCii mpya, kwa kasi kubwa ujenzi.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news