The Royal Tour yawakutanisha Wanadiplomasia, wasomi, makundi yote Dar...Rais Samia asema ni rasmi kwa runinga zote, apongeza

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema, kwa sasa inaruhusiwa kwa runinga na watu wote kuionesha filamu ya The Royal Tour hapa nchini.
Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wageni mbalimbali wakiwa katika uzinduzi wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour katika ukumbi wa Julius Nyerere Conventional Centre leo Mei 8, 2022.

Filamu hiyo ya dakika 56 inaonesha vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania Bara ukiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengenti, hoteli za kitalii ikiwemo iliyopo ndani ya bahari huko Pemba visiwani Zanzibar.

Katika filamu hiyo ambayo uzinduzi wake ulianzia jijini New York,Marekani Aprili 18,2022 Rais Samia Suluhu Hassan ndiye kiongozi wa kutoa maelezo kuhusu vivutio hivyo kwa Peter Grenberg, ambaye ni mwanahabari nguli na mtozi wa filamu kutoka kituo cha televisheni cha CNBC nchini Marekani.
Baadaye uzinduzi huo ulifanyika jijini Los Angeles nchini Marekani, Arusha, Zanzibar na hatimaye leo Mei 8,2022 umefanyika katika Jiji la Biashara la Dar es Salaam nchini Tanzania.

Mheshimiwa Rais Samia akizungumza katika uzinduzi huo amesema, kwa sasa inaruhusiwa kwa runinga zote na watu wote kuionesha filamu hiyo baada ya uzinduzi wake wa mwisho kuhitimishwa leo.

"Tulianza uzinduzi Marekani, Arusha, Zanzibar na leo tunahitimisha hapa Dar es Salaam na kuanzia leo kama alivyosema Katibu Mkuu itakuwa rukhsa kwa TV zote na watu wote kuionesha na iweze kuonekana na Watanzania wote.Nashukuru tumewaletea kitu kitakachobaki kuwa urithi kwa vizazi vya sasa na vijavyo na sio urithi tu wa kuangalia filamu na kuburudika, lakini pia kuutangaza utalii wetu kwa faida za kiuchumi na kijamii,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amewashukuru wadau na Watanzania wote waliotoa michango ya kifedha kufanikisha utengenezwaji wa filamu hiyo.

Sambamba na waliotoa michango mingine ikiwemo mafuta ya magari na makazi kwenye maeneo walipofikia na kulala watu wakati wa uandaaaji wa filamu hiyo

"Niliwaomba watu watuchangie na michango ilienda vizuri, tulikuwa na target (lengo) ya kukusanya shilingi bilioni 20, lakini kwa uwezo wa Mungu tulipata ahadi ya shilingi bilioni 19.39 hizo ni ahadi, lakini jumla ya makusanyo ilikuwa shilingi bilioni 12.759,"amesema Mheshimi Rais Samia.

Amesema,sekta zilizochangia ni Uwekezaji, Uzalishani na Biashara, Sekta ya Fedha na Sekta ya Utalii lakini hao walipitia mabaraza yao.

"Nitoe shukrani za kipekee kwa Dkt.Hussein Mwinyi (Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi)...mwenzangu ambaye jana ilikuwa zamu yake kuionesha pale Zanzibar na jana mambo yalikwenda vizuri,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Pia amesema, kazi itakayoonekana haikuwa rahisi na hapa ilipofikia, "tunamshukuru Mungu na hii imewezekana kwa juhudi zetu za pamoja mimi na nyinyi, kuna wengi waliotoa michango moja kwa moja ya kifedha, ikiwemo mafuta ya magari na wapo waliotupa makazi kwenye maeneo tulipofika na kulala wote nawashukuru,"amesema.
Aidha, amesema filamu hiyo iliyotengenezwa ni mwanzo tu, lakini awamu nyingine zitakuwa zinatengenezwa kwa sababu watengenezaji walichukua picha nyingi za maeneo ya Tanzania.

"Kulikuwa kuna hoja kadhaa kuhusu matumizi ya fedha nataka nikiri kwamba fedha yote tuliyokusanya ndiyo iliyotumika kwenye Royal Tour na tulitumia shilingi bilioni saba kulipa kampuni iliyofanya shooting na kutengeneza filamu nyingine.

"Kuna fedha tulizitumia kwa ajili ya kamati kwenda na kurudi, safari na kila kitu, nataka niwahakikishie bado tuna bakaa, Royal Tour phase 1 ndio hii tunaiona, lakini walio-shoot walichukua picha nyingi sana Tanzania, bado tunakwenda na phase 2 na phase 3, kwa hiyo fedha tuliyonayo tunakwenda kudevelop phase 2 ya Royal Tour na phase 3 ya Royal Tour,"amefafanua Mheshimiwa Rais Samia.

“Sekta ya utalii iko laini sana inapanda na kushuka, hivyo tumeona tuipe nguvu.Wakati wa janga la Covid-19 utalii ulishuka na watanzania wengi walipoteza ajira.Wote tunajua Arusha na Zanzibar inategemea utalii na hata utalii ukiwa chini unaona mambo yalivyokuwa,"amesema.

Mheshimiwa Rais Samia amefafanua kuwa, wakati wa UVIKO-19 watalii na mapato yatoyokanayo na utalii yalishuka.

“Walioathrika zaidi ni waongoza watalii, wenye hoteli, wabebaji watalii , hivyo kutokana na athari hizo wameona ni vema kuutangaza utalii kupitia fimu hiyo. Filamu ilikamilika Machi mwaka huu 2022 na kuanzi mwezi huo vilianza kurushwa vipande vipande ambavyo vimesaidia kuongeza idadi ya watalii pamoja na pato la taifa ambalo limeongezeka kwa asilimia asilimia 48.6,"amefafanua Mheshimiwa Rais Samia.

Mheshimiwa Rais Samia amesema watalii kutoka nje ya Tanzania wamekuja nchini kwa ajili ya kuona vivutio vya utalii na kuongeza filamu hiyo imeonesha hali ya mazingira ya Tanzania na tayari wamepokea maombi kwa kampuni ambazo zinahitaji kaboni baada ya kuona misitu iliyopo hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news