Ujenzi wa Magereza ni muhimu kurahisisha uondoshaji wa mashauri-Jaji Mkuu

NA MARY GWERA-Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa mamlaka husika kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga Magereza katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na maeneo mengine nchini yenye uhitaji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya haki kwa wakati.
Ukaguzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kilindi.

Akizungumza katika siku ya pili ya ziara yake Mahakama-Kanda ya Tanga siku ya Mei 17, 2022 akiwa wilayani Kilindi, Jaji Mkuu, Prof. Juma amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili Wilaya hiyo ni ukosefu wa Gereza hali inayolazimu kutumia Gereza lililopo wilayani Handeni.

“Ukizingatia umbali uliopo kati ya Handeni mpaka hapa ni mrefu, hivyo baada ya kuja hapa leo tunaelewa ugumu ambao wanapata Mahabusu hao kusafiri umbali huo na ukizingatia na hali ya magari ya Magereza, hivyo kwa kuzingatia haki za binadamu ni muhimu kulizingatia suala hili,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Aliongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho Mahakama ya Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya majengo yake ni muhimu pia wadau wa mnyororo wa haki kwenda pamoja na Mahakama ili kuboresha kwa pamoja huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto pamoja na Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto (hawapo katika picha). Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor.

Alisisitiza kuwa Mahakama inaangalia zaidi kuhusu haki ya mtu, hivyo ni muhimu kulichukua suala hili kwa uzito wa kipekee ukizingatia Magereza nyingi ni chakavu kwakuwa zimejengwa kipindi cha ukoloni.

Awali, akitoa taarifa ya Wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe. Abel Busalama amesema kuwa Wafungwa na Mahabusu wenye mashauri katika Mahakama wilayani humo wanapata changamoto kwakuwa umbali ni mrefu takribani kilometa 120 kutoka Handeni.

“Miongoni mwa changamoto ambazo tunakabiliana nazo ni pamoja na Wilaya hii kukosa Gereza, hali hii inaathiri haki za Mahabusu lakini pia kuongeza gharama kwa Serikali kwa kuwasafirisha Mahabusu hao,” ameeleza.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kupata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Gereza hilo. Kadhalika, Mhe. Busalama alimuomba Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma kufikiriwa katika ujenzi wa Mahakama kwakuwa Wilaya hiyo inakabiliwa pia na uhaba wa majengo ya Mahakama.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo, naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi, Mhe. John Chacha alimjuza Jaji Mkuu kuwa mlundikano wa baadhi ya mashauri unachangiwa na umbali wa gereza la Handeni kwa kuwa mahabusu hawaletwi mahakamani kwa muda mrefu hivyo kesi kutosikilizwa kwa wakati.

Mhe. Chacha alisema Mahakama hiyo ina jumla ya mashauri 24 ya muda mrefu ambapo mashauri 21 yapo juu ya mamlaka ya Mahakama ya Wilaya. Jumla ya mashauri matatu Mahakama hiyo ina mamlaka nayo, mashauri mawili (2) ya uhujumu uchumi upelelezi ulikamilika mwezi Aprili, 2022 usikilizwaji wake unaendelea na shauri moja (1) lipo kwenye hatua ya hukumu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto. Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor.

Katika siku ya tatu ya ziara yake, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma anatarajia pia kutembelea Wilaya za Lushoto na Korogwe kabla ya kuhitimisha ziara yake Tanga mjini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news