Watoto 41,000 kupatiwa chanjo ya Polio wilayani Karatu

NA SOPHIA FUNDI

HALMASHAURI ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha inatarajia kutoa chanjo ya matone ya Polio kwa watoto zaidi ya 41,000 chini ya miaka mitano kwa awamu ya pili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo mganga mkuu wa wilaya,Dkt.Lucas Kazingo amesema kuwa, chanjo hiyo itatolewa kuanzia Mei 18 hadi Mei 21, 2022 katika vituo vyote vya afya vya wilaya pamoja na zahanati.

Amesema kuwa, pamoja na chanjo kutolewa katika vituo vya afya pia kutakuwa na timu ya wataalam itakayozunguka nyumba kwa nyumba itakayoongozwa na wenyeviti wa vitongoji ambao watatoa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano watakaokutwa katika nyumba hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkuu wa wilaya ambaye ni afisa tawala, Bi.Jacgueline Rwezaula amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto katika zoezi la chanjo ambayo imekwishazinduliwa na kuwahakikishia wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama.
Amesema kuwa, lengo la kampeni ni kuongeza kinga ya mwili kwa watoto chini ya miaka mitano na hivyo kuzuia kuenea kwa maambukizi ya kirusi cha polio kilichoripotiwa nchi jirani ya Malawi.

Naye mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Sally Emanuel aliwaomba wananchi kuepuka upotoshaji kuhusiana na chanjo ya polio inayotolewa kwani chanjo hiyo ni salama.

Amewasihi wananchi pale wanapomuona mtoto anadalili yoyote ya ugonjwa huo waripoti hospitali Ili apatiwe huduma ya afya kabla hajaambukiza wengine.
Pia akizungumza na wananchi mwakilishi wa ofisi ya mganga mkuu wa mkoa, Denis Mgiye aliwaomba wananchi kujitokeza kuwapeleka watoto kwenye chanjo hata kama walipata chanjo hiyo kwenye kliniki, kwani kutokana na mlipuko huo ulioko nchi jirani ni lazima watoto wote chini ya miaka mitano wapewe chanjo hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news