Dodoma Jiji yapewa kongole kwa ubunifu, ukusanyaji mapato

NA DENNIS GONDWE

TIMU ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma (CMT) imepongezwa kwa kazi nzuri katika makusanyo ya mapato ya ndani na kukumbushwa kusimamia taratibu za utumishi ili uweze kuwa na mafanikio. 
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga alipokuwa akiongea na CMT ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo leo.

Dkt. Mganga alisema “niwapongeze CMT yenu kwa ukusanyaji mzuri wa mapato. Nyie si watumishi tu, bali ni viongozi. Kupata neema ya uongozi si masihara. Wakuu wa idara mnatakiwa kumsaidia mkurugenzi kutekeleza majukumu yake kwa kusimamia taratibu na sheria za utumishi wa umma”. 

Aidha, aliwataka wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya vikao vya kazi wa wafanyakazi walio chini yao ili kujadili utendaji kazi. 

“Ni vizuri migao ya fedha za matumizi ya kawaida ziwekwe wazi kwa watumishi wote na siyo viongozi kugawa wenyewe bila wafanyakazi waliochini yenu kuwa na taarifa. Uwazi wa kushirikishana katika utendaji kazi, uwazi huwa unasaidia kupata usaidizi wa mawazo na kuyasimamia. Tubadilike katika eneo hili, kila mmoja apangiwe kazi kwa uwazi na kupimwa utendaji wake na kupongezwa utekelezaji wake,”alisema Dkt. Mganga. 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa lengo la CMT ya jiji hilo ni kutoa huduma bora kwa wananchi. 

“Sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wananchi wote ni wetu na tuna wajibu wa kuwahudumia. Niishukuru TAMISEMI na Ofisi yako kwa kutupatia watumishi wazuri. Mimi kwenye timu yangu sioni mtumishi ambae ni mzigo. Ndugu Katibu Tawala Mkoa nikuhakikishie kuwa ndani ya miezi michache utaona matokeo ya kazi. Tupo vizuri kwenye magari na tumeagiza mitambo ambayo itaingia mwezi Julai. Tunataka tabia hii ya utendaji wa kazi wa CMT tuihamishie kwa wafanyakazi walio chini yetu,” alisema Mkurugenzi Mafuru.

Katibu Tawala Mkoa alifanya ziara katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuongea na CMT na Wafanyakazi kwa nyakati tofauti ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza tarehe 16-23 Juni, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news