Mwenyekiti CCM Mara: Ni jukumu letu viongozi, wadau kuhamasisha Sensa Agosti 28 kwa maendeleo

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara,Samwel Kiboye (Namba Tatu) amewashauri viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini,kiserikali, kisiasa, kimila na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Mara kuendelea kuhamasisha wananchi mkoani humo ili waweze kujiandaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Ameyasema hayo leo Juni 20, 2022 wakati akizungumza na DIRAMAKINI kuelezea kuhusu umuhimu na nafasi ya viongozi katika nafasi zao kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23,2022.

Kiboye amesema,ushiriki wa wananchi wote katika sensa hiyo utaisaidia Serikali kufahamu namna bora ya kutenga rasilimali fedha na miradi mbalimbali ya maendeleo na kuielekeza huko walipo iweze kuleta tija.

"Chukua mfano hata nyumbani kwako, kila unapotaka kufanya bajeti ya familia lazima izingatie idadi na mahitaji ya waliopo katika familia, kwa maana ya mama, baba, watoto na ndugu ambao pengine upo nao nyumbani, ukishaainisha mahitaji hayo, unafahamu ni wapi pa kuanzia ili uyatekeleze.

"Hivyo,ndivyo ilivyo hata kwa Serikali inapotaka kupanga mambo yake inahitaji ifahamu kama ni huduma za maji, vituo vya afya, elimu au miundombinu ya barabara ielekeze wapi? Pengine inataka ipeleke huduma hizo mahali ambapo mahitaji si makubwa kulingana na eneo fulani ambalo lina wingi wa watu, hivyo inapopata takwimu sahihi za watu zinasaidia kutoa dira kamili juu ya kufanikisha hilo,"amefafanua Kiboye.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Pia taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mara amesema kuwa,mafanikio ya Sensa ya Agosti 23, 2022 katika maeneo yote ya mijini na vijijini ni ishara njema ya kuisaidia Serikali kufahamu hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote.

"Jambo lingine, kwetu sisi wana siasa Sensa hii ni ya muhimu sana kwa sababu inajenga msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa kidemokrasia kwa maana gani? Kila mmoja wetu amesikia NBS wakisema wazi kuwa, takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa, hivyo ni jukumu letu kuhamasisha wananchi wetu kujiandaa kuhesabiwa Agosti 23, 2022,"amesema Kiboye.

Aidha,Kiboye amewataka wananchi siku ya sensa kuwapa ushirikiano wa kutosha makarani wa sensa kwa kuwa, taarifa zao si kwa manufaa yao tu, bali kwa jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

"Makarani wa sensa wakifika tusisite kuwapa taarifa zote sahihi kulingana na maswali watakayouliza kuanzia takwimu zetu wenyewe hadi makazi yetu, ninaposema makazi ninamaanisha nyumba zetu ili kulifanya zoezi hilo kuwa jepesi na utekelezaji wa malengo ya Serikali uweze kufanikiwa kwa haraka,"amesema Kiboye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news