Nitatekeleza ahadi na juhudi zinaendelea asema Rais Dkt.Mwinyi

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba, juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi zinatekelezwa ipasavyo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Sheikh.Khamis Mussa Khamis (kushoto kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Fumba Bondeni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 17-6-2022.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Ijumaa Fumba Bondeni, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi. 

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, anaamini kwamba bado changamoto za kimaendeleo zipo, lakini juhudi zitaendedea kuchukuliwa usiku na mchana na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia wananchi wa Kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi “B” Unguja baada ya kumalizika kwa Ibaada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Fumba Bondeni leo 17-6-2022.(Picha na Ikulu). 

Hivyo, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwasihi waumini wote nchini kuendelea kuomba dua ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu kuweza kutekeleza yale aliyoyaahidi. 

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwaahidi waumini wa Msikiti huo wa Ijumaa Fumba Bondeni kuzipatia ufumbuzi changamoto zao zinazowakabili ambazo walizitoa mbele yake ikiwemo huduma ya maji safi na salama. 
Wananchi wa Kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi “B” Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na kuwasalimia baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Fumba Bondeni leo 17-6-2022.(Picha na Ikulu) 

Naye Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Mfaume aliwasisitiza waumini wote nchini kuendelea kumuombea dua Rais Dkt. Mwinyi ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani ana kazi kubwa ya kuwaongoza wananchi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo endelevu. 

Sambamba na hayo, Sheikh Khalid aliwataka waumini kuhakikisha wanazitumia vyema ndimi zao kwani ni miongoni mwa viungo ambavyo kiongozi wa Waislamu Mtume Mohammad (S.A.W), amesisitiza vitumiwe vizuri ili kuepuka na adhabu za Mwenyezi Mungu huku akisisitiza kusema na kutenda yaliyomazuri. 

Mapema akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Maulid Issa Shani aliwasihi waumini wa dini ya Kiislamu kuendelea kufanya mambo mema kwani kila analofanya mja ninajulikana na linaandikwa na hatimae atalipwa kwa jema ama ovu alilolifanya. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuagana na Sheikh.Khamis Mussa Khamis, baada ya kumaliza Ibaada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Fumba Bondeni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja iliyofanyika leo.(Picha na Ikulu). 

Pamoja na hayo, Sheikh Maulid Issa Shani katika hotuba yake hiyo alieleza kwamba Mwenyezi Mungu atawalipa waja wake kutokana na amali zao walizozifanya duniani hivyo, alisisitiza haja ya kuendelea kutenda mambo mema na kuepukana na kutenda maovu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news