RC MWANZA:WARATIBU WA SEQUIP TIMIZENI NDOTO ZA ELIMU KWA WASICHANA WALIOKATISHA MASOMO

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewataka waratibu wa Mradi wa Sequip unaolenga kuwapa fursa wasichana waliokatisha masomo ya Elimu ya Sekondari kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kuzingatia maagizo ya mradi huo ili kuhakikisha malengo yanatimia.
Mkuu wa Mkoa amebainisha hayo Juni 14, 2022 alipokuwa akifungua Warsha ya Siku 4 ya kuwajengea uwezo waratibu na wawezeshaji 75 wa Vituo vya Mradi wa Sequip chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu wazima kutoka Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Kigoma, Manyara Shinyanga, Simiyu na Tabora ya katika Ukumbi wa Butimba TTC.
"Nampongeza sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jambo hili maana kundi la mabinti waliokosa Elimu kwa sababu mbalimbali limepitia kwenye msukosuko mkubwa hivyo kuwaona na kuamua kuwasaidia ni jambo kubwa na lenye baraka mbele ya Mungu,"amesema RC Gabriel.
Dkt.Belingtone Mariki, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya watu Wazima amesema kuwa mradi huo pamoja na mambo mengine umelenga kuwawezesha wasichana elfu tatu walioacha Masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo Ujauzito na kwa mwaka huu wamesajiri wasichana 3333 na walimu 802 watahusika ambapo Mkoa wa Mwanza una Vituo 14 vyenye wanafunzi 241.
"Sisi kama Taasisi tunaishukuru sana serikali kwa kutoa fursa hii ya kuhakikisha ndoto ya kupata elimu kwa mtoto wa kike inatimia kwani kupitia mradi huu tunaamini malengo ya Kumuinua mwanamke kiuchumi pia utatimia,"Prof.Sotko Komba, Makamu Mwenyekiti Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu a Watu Wazima.
Mkufunzi Mkazi wa Mwanza kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Ritha Kakwira amemshukuru Mkuu wa Mkoa na amemhakikishia ushirikiano na Ofisi yake wakati wote katika utekelezaji wa mradi huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news