Serikali yawafahamisha Wanadiplomasia walioko nchini juu wananchi walioamua kuhama kwa hiyari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Waziri Balozi Mulamula asisitiza jambo

NA WAANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa nchini kuwa inazingatia na kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu huku ikiendelea kulinda uhifadhi wa eneo la Ngorongoro.
Baadhi ya Mabalozi katika picha ya pamoja na meza kuu baada ya kikao kati ya Serikali na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo Jijini Dar es Salaam alipozungumza na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuuhakikishia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania inazingatia na kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu na hakuna nanma itaendesha mipango yake kwa kukiuka sheria za haki za binadamu,”alisema Balozi Mulamula.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (hawapo pichani) kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mpango wa kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro nchini kwa wananchi kuridhia kuhama kwa hiari yao na kwamba hakuna aliyeondolewa katika eneo hilo kwa nguvu kama inavyoelezwa.

“Tanzania siku zote italinda watu wake, maliasili zake na mipaka yake kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” alisema Balozi Mulamula.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

Akizungumza katika kikao hicho maalum kwa ajili ya kuielezea Jumuiya ya Kimataifa iliyopo nchini, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kinachoendelea katika eneo la Ngorongoro kwa wakati huu ni uhamaji wa hiari wa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la Ngorongoro na sio kwamba kuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa na Serikali.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza katika kikao na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (hawapo pichani) kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

“Serikali imekuja na mpango wa kulinda eneo la Ngorongoro, imechukua miaka 20 kuandaa na kuratibu mpango huu, ambao unatekelezwa sasa na hakuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa kwa wanachi kama inavyodaiwa, wananchi husika wameshirikishwa vya kutosha na ndio maana wamekubali na kuamua kuhama kwa hiari wenyewe,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Amesema Katiba ya Tanzania inasema watu wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kuishi popote na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu wananchi wake wote bila ya kujali rangi, kabila au dini zao.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akimkaribisha Waziri wa mambo ya Nje kuzungumza na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (hawapo pichani) kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

Amesema, wananchi wamepewa umiliki kwa miaka kadhaa na endapo itaonekana kuna haja ya kuichaukua ardhi hiyo anayeimiliki hulipwa fidia na kupewa ardhi katika eneo lingine na kuongeza kuwa wananchi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro wanalipwa fidia na kupatiwa nyumba za makazi, maeneo yenye huduma za kijamii na ardhi kwa ajili ya malisho ya mifugo. 

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema kwamba katika wilaya ya Ngorongoro kuna maeneo mawili ambayo yamekuwa yakizua mjadala ambayo ni eneo la hifadhi la Ngorongoro ambalo ni urithi wa dunia na Pori Tengefu la Loliondo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja akizungumza na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (hawapo pichani) kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

Amesema, Serikali imechukua uamuzi wa kutekeleza mpango huo kutokana na changamoto kadhaa ambazo zinatishia uhifadhi wa eneo la Ngorongoro na kuongeza kuwa uhamaji wa hiari unaofanyika katika eneo la Ngorongoro una lengo la kuendelea kuhifadhi eneo hilo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Akizunguma katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela amewahahakikishia wanadiplomasia nchini kuwa zoezi hilo lilihusisha wananchi wa jumuiya zote waliokuwa wakiishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuahidi kuwa majadiliano bado yanaendelea ili kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na uelewa wa pamoja katika suala hilo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa azma ya uhifadhi wa hifadhi ya Ngorongoro.
Balozi wa Visiwa vya Comoro Nchini, Dkt. Ahmada El Badaoui Mohammed akitoa salamu za shukrani baada ya kikao kati ya Serikali na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (hawapo pichani).
Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiwakaribisha Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa katika mkutano.
Mkurugenzi wa Diaspora, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akifuatilia mkutano kati ya Serikali na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa.
Balozi wa Ufaransa Nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui akichangia katika kikao kati ya Serikali na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini (hawapo pichani) kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.

Mkutano huo uliohusisha viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Wizara za mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Maliasili na Utalii, Katiba na Sheria pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Arusha na Tanga.

Mkutano huo ulilenga kuwafahamisha wanadiplomasia walioko nchini juu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhama kwa hiari kunakofanywa na wananchi waliokuwa na makazi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na hivyo kuondoa sintofahamu iliyokuwepo kuwa wananchi hao wanahamishwa kwa nguvu na serikali na hivyo kukiuka haki za binadamu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news