Tanzania yapiga hatua huduma jumuishi za fedha, Waziri Dkt.Nchemba awashirikisha viongozi fursa zilizopo nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amewahakikishia viongozi wa Kanda ya Afrika wa Taasisi ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI) kuwa, Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii na fursa nyingi za uwekezaji, hivyo waone umuhimu wa kuangalia ni eneo gani ambalo watakwenda kuwashirikisha wawekezaji kutoka nchini mwao ili kuja kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba ametoa rai hiyo kwa njia ya mtandao wakati akifungua Mkutano wa Kanda ya Afrika wa Taasisi ya Huduma Jumuishi za Fedha  uliondaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion) katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha leo Juni 23,2022.
"Kwa mara nyingine tena niwakaribishe nchini Tanzania na ninawasihi msifanye hii kuwa ziara yenu ya mwisho katika nchi yetu pendwa ya Tanzania. Mbali na kuwa na vivutio vya kuvutia vya kitalii kama vile Mlima Kilimanjaro, Kreta ya Ngorongoro na fukwe za asili na za kisasa huko Zanzibar na Mafia, Tanzania pia ni nchi ya kimkakati kwa uwekezaji. 

"Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikijumuisha migodi, ardhi yenye rutuba na vyanzo vya maji mengi kwa ajili ya kilimo pamoja na maeneo ya kimkakati ya viwanda. Niwaombeni mkiwa hapa,tumieni pia muda wenu kuchunguza fursa za uwekezaji na msisite kufadhili wawekezaji kutoka nchini mwenu wakati wanapanga kuwekeza Tanzania. 

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tuko tayari kuwapa ushirikiano wa kutosha kupitia mamlaka zetu hususani kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania na pia kupitia wizara zetu,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba wakati akifungua mkutano huo wa 10 kwa viongozi hao barani Afrika.

Kupitia mkutano huo ambao umewajumuisha Magavana wa Benki Kuu, Manaibu Magavana na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, Mheshimiwa Waziri.Dkt.Nchemba amesema kuwa, "Wakati mkijadili kuhusu mada ya “Africa’s leadership on inclusive finance through digitization for stability and growth”, Tanzania ina mengi ya kusema juu ya umuhimu wa teknolojia ya digitali katika kukuza ushirikishwaji wa kifedha na maendeleo ya kiuchumi; 

Hatua muhimu

Mheshimiwa Waziri amesema, kwa upande wa kufanya miamala ya fedha kwa njia ya simu za mikononi kuna hatua ambayo wamepiga.
"Mwaka 2006, Tanzania ilifanya utafiti wake wa kwanza wa Finscope ambapo ilionekana ni asilimia 46 tu ya watu wazima walijumuishwa katika huduma za kifedha, ambapo ni asilimia 11 tu, walikuwa wanatumia huduma rasmi za kifedha. Sababu kuu za kutengwa zilikuwa eneo kubwa la kijografia na mawasiliano duni katika maeneo ya vijijini na utoaji wa gharama kubwa kwa huduma za kibenki.

"Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali iliamua kuweka mazingira wezeshi yatakayohimiza uwekaji wa huduma za kifedha katika mfumo wa kidigitali. Pia iliruhusu taasisi zisizo za kibenki (Telecoms) kutoa huduma za malipo. 

"Kwa hiyo, mapema mwaka wa 2008, kampuni inayojihusisha na teknolojia ya masuala ya kifedha, E-Fulusi ilizindua mfumo wake wa kwanza nchini Tanzania, MobiPawa, muda mfupi baadaye ukafanyika uzinduzi wa M-Pesa na Vodacom mwezi Aprili 2008. Miaka miwili baadaye, kampuni nyingine tatu za simu zikazindua huduma za Z-Pesa (Zantel), Airtel Money (Airtel), Tigo Pesa (Tigo) na baadaye T-Pesa (TTCL),"amefafanua Mheshimiwa waziri Dkt.Nchemba.
Amesema, kuanzishwa kwa huduma hizo za kifedha kwa njia ya simu, pamoja na huduma za benki kwa wakala na benki kwa njia ya simu, kuliongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini, na kupunguza gharama za miamala ya kifedha.

Hivyo kupunguza idadi ya watu ambao wametengwa katika sekta ya fedha. Hii inathibitishwa na matokeo ya tafiti za Finscope zilizofanyika mwaka 2013 na 2017, ambapo uwiano wa watu waliojumuishwa kifedha kwa huduma rasmi za kifedha ulikuwa asilimia 57 na asilimia 65.

"Kwa maana ya wanawake na wanaume, ikumbukwe kuwa, kati ya watoa huduma rasmi za kifedha waliotambuliwa kupitia Finscope 2017, asilimia 48.6 walikuwa wanaingia kupitia simu ya mkononi. 

"Mwaka 2021, thamani ya miamala ya fedha kwa njia ya simu kwa jumla ya Pato la Taifa iliongezeka hadi asilimia 66 kutoka asilimia 40 mwaka 2013. Wakati huo huo, watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu ilikuwa milioni 35.3 mwezi Desemba 2021, sawa na asilimia 61 ya watu wote nchini Tanzania,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Gavana BoT

Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Prof. Florens Luoga amesema kuwa, mkutano huo umewakutanisha viongozi mbalimnbali kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion) lengo likiwa ni kuangalia jinsi gani huduma jumuishi za kifedha zinawafikia wananchi kwa urahisi ili kuharakisha maendeleo.
"Hivyo, tunakaa kila baada ya muda kuweza kuangalia na kujipima tumefikia wapi, tumepambana na changamoto zipi katika kuhakikisha huduma jumuishi za kifedha zinatumika ama zinafanikiwa kuleta maendeleo ya wananchi wa kawaida, sisi katika Benki Kuu tulichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanafikiwa.

"Kwa mfano lengo la Tanzania ni kuhakikisha kila mwananchi pale alipo anatembea si zaidi ya kilomita 15 bila kukuta huduma ya kifedha, tumejizatiti mabenki yetu kupeleka huduma kupitia kwa mawakala, pili kuhakikisha makampuni yetu ya simu yanatoa huduma za kifedha, tatu hizo huduma lazima zitolewe kwa gharama ambazo sio ghali.

"Gharama ambazo zitawafanya walengwa ambao ni wananchi ambao walikuwa hawapati huduma za kibenki kuzipata na hawa walikuwa ni wengi sana,"amesema Prof.Luoga.

Prof.Luoga amesema, kwa upande wa Tanzania huduma jumuishi za kifedha zimewafikia wengi na wanataka huduma hizo ziweze kuwa na tija ili kubadilisha maisha.

Pia amesema, lengo lao ni kuhakikisha huduma za kifedha kupitia mtandao ziwawafikia walengwa bila kuwaathiri ama kuwakosesha uwezo wa kuzipata popote pale nchini.

Dkt.Hannig

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), Dkt.Alfred Hannig amesema kuwa,kupitia huduma za AFI ambazo zinategemea kujifunza na kubadilishana ujuzi, pamoja na usaidizi wa kiufundi, ushirikiano na kuwajengea uwezo, wanachama wa AFI barani Afrika wameripoti zaidi ya mabadiliko 150 ya sera kati ya 2019 na 2021 katika maeneo matatu muhimu.

Amesema, maeneo yaliyoripotiwa mwaka 2021 na taasisi wanachama wa AFI barani Afrika ni huduma za kifedha za kidijitali, ujumuishaji wa kifedha wa kitaifa na mkakati wa fedha kwa wafanyabiashara ndogo na wa kati (SMEs).

Pia amesema, umefika wakati sasa wa kulinda maslahi ya Afrika katika mazungumzo ya kimataifa na kuhakikisha usawa unatawala kupitia wadau husika katika hatua zote.

Amesema, ushirikiano huo unalenga kuimarisha juhudi mbalimbali za upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha barani Afrika ili kuwanufaisha wananchi katika ngazi zote.

Akielezea kuhusu AfPI ambalo ni jukwaa la msingi kwa wanachama wa AFI barani Afrika amesema, linaunga mkono na kuendeleza sera za ujumuishi wa kifedha na mifumo ya udhibiti, na kuratibu juhudi za kikanda za kujifunza. 
Dkt.Hanning anasema,Jukwaa la AfPI linaleta pamoja wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka taasisi za utungaji sera za kifedha na udhibiti za Afrika ili kuimarisha utekelezaji wa sera bunifu za ujumuishaji wa kifedha katika bara zima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news