WATUMISHI NEC WACHANGIA DAMU, WAFANYA USAFI HOSPITALI YA UHURU DODOMA

NA MWANDISHI WETU

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma nchini ambayo kila mwaka hufanyika kuanzia tarehe 16 -23 Juni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imechangia damu na kufanya usafi katika Hospitali ya Uhuru iliyopo katika wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Watumishi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi wameshiriki utoaji wa damu ikiwa ni kuunga mkono jitihada za kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa, akina mama wajawazito na watoto.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chamwino, Dkt. Abdul Pumzi amesema uhitaji wa damu katika hospitali zetu nchini ni mkubwa mno, hivyo amewapongeza watumishi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kujitoa kwao kwa kuchangia damu kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Uhuru Chamwino, Dkt.Abdul Pumzi akizungumza na Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mara baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi na Uchangiaji wa Damu lililofanyika Hospitali hapo tarehe 16 Juni,2022.
"Ni furaha kuwaona watumishi wa umma kama nyinyi mkishirki na kuunga mkono uchangiaji wa damu. Tumekuwa tukizunguka mijini na vijijini kuhimiza uchangiaji wa damu na hii ni kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa sana kwenye hospitali zetu. Kuna wa kina mama wajawazito, kuna majeruhi wa ajali mbalimbali, kuna watoto, wote hawa wana uhitaji wa damu, hivyo kuja kwenu hapa ni ishara ya moyo wa upendo," alisema Dkt.Pumzi.

Awali akizungumza na Watumishi wa Tume, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Uhuru Bi. Joyce Nchimbi aliupongeza uongozi wa Tume kwa kuwafikiria na kufika katika hospitali hiyo na kushiriki zoezi la usafi na uchangiaji wa damu kama sehemu ya kuadhimisha kuadhimisha wiki ya utumishi wa Umma. 

Alitoa wito kwa taasisi na mashirika binafsi kujitoa kwa namna hiyo ili kuokoa maisha ya wagonjwa walio wengi katika hospitali zetu nchini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Leonard Tumua amesema ushiriki wa watumishi katika uchangiaji wa damu na ufanyaji wa usafi katika wiki hii ya utumishi wa Umma unalenga kujenga mahusiano mema kati ya wadau ambao ni wananchi na Tume ya Taifa ya uchaguzi.

"Sisi kama Tume tunafanya kazi na wadau mbalimbali, hivyo kushiriki katika mazoezi kama haya, kunatuweka karibu na wadau wetu ambao ni wananchi, kunadumisha mahusiano mema na upendo miongoni mwetu sote,"alisema Bw.Tumua.
Nao baadhi ya watumishi kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi walioshiriki zoezi hilo wamesema, wamefurahishwa na uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwaruhusu kushiriki zoezi la ufanyaji wa usafi lakini pia kutoa damu ikiwa ni ishara ya upendo wa watanzania waliopo hospitali na wenye uhitaji wa Damu.

"Tunashukuru sana uongozi wetu ukiongozwa na Dkt. Wilson Mahera Charles kwa kuona umuhimu wetu kama watumishi kushiriki katika shughuli za kijamii hasa uchangiaji wa Damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa,”alisema Bw. Erasto Mwakalinga.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma imeanza tarehe 16 mwezi Juni na inatarajia kumalizika Tarehe 23 mwezi Juni 2022 huku ikiwa na ujumbe Nafasi ya Mapinduzi ya nne ya Viwanda katika masuala mapya yanayojitokeza kuhusu utoaji wa huduma na urejeshaji wakati na baada ya janga la Corona.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news