Waziri wa Nishati afanya mazungumzo na Mwakilishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza

NA TERESIA MHAGAMA

WAZIRI wa Nishati, Mhe.January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na Balozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabia nchi Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Janet Rogan ambaye amemwakilisha Rais wa Mkutano wa 26 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza.
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (kulia) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabia nchi Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Janet Rogan (wa Pili kulia). Wengine katika picha ni Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar (Wa tatu kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, na Watendaji kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.

Mkutano wa viongozi hao umefanyika jijini Dodoma tarehe 23 Juni, 2022 na kuhudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali pamoja na watendaji wengine kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.

Majadiliano ya viongozi hao yalihusu mabadiliko ya tabia nchi pamoja na jinsi Tanzania ilivyojipanga katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 26 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi uliofanyika mwaka 2021 nchini Uingereza ambapo Tanzania ni Nchi mwanachama.
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabia nchi Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Janet Rogan baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi. Kushoto ni Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar.

Baadhi ya maazimio ya Mkutano huo wa COP26 ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala, matumizi ya umeme kwenye magari pamoja na kupunguza ukataji miti.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba, alimweleza Balozi huyo kuwa, Tanzania inafanya juhudi mbalimbali kutekeleza maazimio hayo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala mijini na vijijini pamoja na magari kutumia gesi asilia na umeme.
Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba (Wa Pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabia nchi Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Janet Rogan (Wa Tatu kulia) baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi. Wengine katika picha ni Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar (wa Tatu kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (wa kwanza kulia), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa kwanza kushoto) na Watendaji kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.

Aidha, alimweleza Balozi huyo juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na nishati ya kutosha kwa kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo Jotoardhi, Jua na Gesi Asilia.

Pia alimweleza kuwa, Serikali ipo mpango wa kuandaa na kuboresha mikakati mbali ya kisekta pamoja na kuboresha mfumo wa gridi ya Taifa ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na nishati ya uhakika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news