Tanzania yaipongeza AfDB kwa kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo

Serikali ya Tanzania imeishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuendeleza ushirikiano wao wa muda mrefu katika kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ukiwemo mkopo wa masharti nafuu wa dola miloni 120 ulioridhiwa Jumatano wiki hii kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa umeme kutoka mto Malagarasi,anaripoti Farida Ramadhani na Ramadhani Kissimba (WFP) Dar es Salaam.

Shukrani hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt. Philip Isidor Mpango wakati akimuaga aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini, Dkt. Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango (kulia) akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), nchini Dkt. Alex Mubiru (kushoto), alipokuwa akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu mjini Abidjani, Ivory Coast.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango (kulia) akimkabidhi zawadi ya picha ya utalii, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Dkt. Alex Mubiru (kushoto), alipokuwa akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu mjini Abidjani, Ivory Coast. 

Dkt. Mpango amesema kuwa mradi huo wa bwawa kubwa la umeme unatarajiwa kuzalisha takribani megawati 49.5 za umeme kwa ajili ya Mkoa wa Kigoma na mikoa ya jirani.

Amesema, Dkt. Mubiru kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika amesaidia kusukuma fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati hapa nchini na katika miaka miwili aliyokaa hapa, Tanzania imeweza kunufaika na fedha za kutekeleza miradi yenye thamani ya takriban dola bilioni 2.5.

“Miradi mingine iliyotekelezwa na benki hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu jijini Dodoma ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, barabara za mzunguko katika jiji la Dodoma na kituo kikubwa cha umeme cha Zuzu,”amesema.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango (kulia) akimkabidhi zawadi ya kitabu Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Dkt. Alex Mubiru (kushoto), alipokuwa akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu mjini Abidjani, Ivory Coast.

Dkt. Mpango ameitaja miradi ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 260 kutoka Manyovu, Buhingwe, Kasulu hadi Kabingu mkoani Kigoma pamoja na mradi wa kuunganisha Mkoa huo na umeme wa gridi kuu ya Taifa kuwa ni miongoni mwa miradi mingine iliyotekelezwa kwa mikopo ya AfDB.

Aidha, Dkt. Mpango amemuomba Dkt. Mubiru kufikisha salamu za Serikali ya Tanzania na watanzania kwa ujumla kwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kubainisha kuwa anaamini Mwakilishi Mkazi atakayeteuliwa atakuja kuendeleza pale walipoishia.Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), nchini Dkt.Alex Mubiru (kushoto), akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango(kulia) alipokuwa akiagwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu Jijini Abidjani, Ivory Coast.

Naye aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa benki hiyo nchini, Dkt. Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo, alisema anaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha miaka miwili alipokuwa nchini.

Ameipongeza Serikali kwa kupiga hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kubainisha kuwa Tanzania inauthubutu wa kipekee linapokuja suala la maendeleo.

Amesema, kwa niaba ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news