Mbaroni kwa tuhuma za kuongoza genge la uhalifu Dar

Mfanyabiashara, Sadikiel Meta (71) na wenzake 14 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kuwatumikisha walemavu na kuwafanya kuwa ombaomba, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mengine ni usafirishaji haramu wa binadamu, kutakatisha fedha, kukwepa kulipa kodi na ba kuisababishia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasara ya zaidi ya sh. milioni 31.3

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon imewataja washtakiwa wengine kuwa ni Yusuph Mohamed (35), Yusuph Magadu (20), Emmanuel Salu (20) Gogad Mayenga (18), Samson Taruse (26), Hussein John (18), Zacharia Paul (18), Dotto Shigula (19), Petro Simon (21), Emmanuel Sahani (38), Joseph Mathias (20), Masanja Paul (21), Aminiel Sangu (19), na Emmanuel Lusinge.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Kassian Matembele imedaiwa katika tarehe tofauti za Agosti 2020 na Januari Mosi 2021 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walishiriki kufanya uhalifu wa kupanga kwa kuongoza genge la uhalifu na kutekeleza kufanikisha kusafirisha binadamu kwa haramu.

Katika shitaka la pili la usafirishaji haramu wa binadamu inadaiwa, katika kipindi hicho hicho huko Tandale ndani ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mshtakiwa Meta na Mohamed waliwatumikisha walemavu 37 na kuwafanya wawe ombaomba wa mtaani kwa lengo la kujipatia kipato.

Miongoni mwa walemavu hao ni mtoto Kashinje Emmanuel (7),Doto Silas Happines Bezagurwa, Neema Edward na Peter Sereke wote wa ama umri wa miaka 11.

Imedaiwa wa washtakiwa hao pia walikuwa wakisafirisha walemavu kutoka mikoa ya Shinyanga na Tabora kwenda Dar es Salaam na kwamba wakishapokelewa wanawaingiza kwenye shughuli za ombaomba kwa lengo la kujipatia faida.

Aidha, mshtakiwa Meta anadaiwa kushindwa kulipa kodi ya thamani ya sh. milioni 31,328,500.31 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).Pia mshtakiwa Meta anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh.milioni 31.3.

Katika shtaka la mwisho la utakatishaji imedaiwa kati ya Agosti 2020 na Januari Mosi 2021, mshtakiwa Meta alijipatia sh.Milioni 31,328,500.31 huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kushindwa kulipa kodi.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Januari 26,mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments