Polisi, raia kizimbani wakikabiliwa na mashitaka sita

Askari watatu na raia watano akiwemo mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite jijini Arusha,Lucas Mdeme (46) mkazi wa Njiro wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha wakikabiliwa na mashtaka sita, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Miongoni mwa mashitaka hayo ni pamoja na uhujumu uchumi,utakatishaji fedha haramu na kupanga njama za kujipatia fedha ya awali shilingi milioni 10 kati ya shilingi milioni 30 walizohitaji kutoka kwa Sammy Mollel. 

Askari watatu waliofukuzwa kazi kwa tuhuma ya rushwa na kupandishwa kizimbani ni pamoja na namba G. 5134 DC Heavenlight Mushi aliyekuwa askari Kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni jijini Dar es Salaam,H.125 PC Gasper Paul aliyekuwa Kitengo cha Intelijensia makao makuu Dodoma na H.1021 PC Brython Murumbe aliyekuwa askari wa kawaida mkoani Dodoma. 

Raia waliopandishwa kizimbani mbali ya Mdeme wengine ni pamoja na Joseph Chacha (43) au Baba Ngodo mkazi wa Ilboru,Leonila Joseph (46) mkazi wa Ilboru,mfanyabishara maarufu jijini Arusha, Nelson Lyimo(58) mkazi wa Kijenge Juu na Omary Alphonce (43) au Matelephone mkazi wa Olasiva jijini Arusha. 

Wakisomewa mashtaka na waendesha mashtaka waandamizi wa Serikali,Adelaide Kassalay na Agnes Hyera mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Arusha,Rose Ngoka walidai kuwa shitaka la kwanza linawakabili mshitakiwa wa 1,2,3 ambao ni askari kuwa Desemba 5, 2020 walijihushisha na uhalifu huku wakitambua kuwa wao ni watumishi wa umma na kujipatia rushwa ya awali ya kiasi cha shilingi milioni 10 kutoka kwa Sammy Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Gems and Rock Venture ya jijini Arusha. 

Kassalay amesoma shitaka la pili linalowakabili washitakiwa wanne ambaye ni Baba Ngodo,mshtakiwa wa tano Joseph ,mshtakiwa wa sita Lyimo,mshtakiwa wa saba Mdeme na mshtakiwa wa nane Matelephone wote wanashitakiwa kwa kujifanya watumishi wa umma na kuunda mtandao wa kihalifu na kupanga njama za kujipatia fedha taslimu shilingi milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Mwendesha mashitaka huyo amesoma shitaka la tatu linalowakabili watuhumiwa wote nane ambalo ni la kupanga njama za kuhujumu uchumi, kwani Desemba 5, 2021 waliweza kujipatia fedha shilingi milioni 10 kutoka kwa Mollel. 

Amesema shitaka la nne linamkabili Chacha mshitakiwa wanne ambaye anatuhumiwa akiwa na nia kufanya uhalifu na udanganyifu na kujitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa umma Ikulu. 

Mwendesha mashitaka huyo amesoma shitaka la tano linalowahusisha washitakiwa wote kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni 10 za awali kati ya shilingi milioni 30 ili wamwachie huru kwa tuhuma za kukwepa kodi na kufanya biashara ya madini ya Tanzanite kwa kutorosha madini nje kinyume cha sheria. 

Kassalya amesoma shitaka la sita la utakatishaji fedha haramu linalowakabili washitakiwa wote kwani ilidaiwa mahakamani hapo kuwa wote kwa pamoja Desemba 5, 2021 walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu shilingi milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara Sammy Mollel. 

Hata hivyo, mara baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Ngoka amewaeleza watuhumiwa wote kuwa hawatakiwi kujibu chochote, kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashitaka hayo na watuhumiwa mtaenda rumande hadi Januari 27, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

Post a Comment

0 Comments