Rais Dkt.Mwinyi:Tutazingatia mahitaji ya wazee ikiwemo makazi, afya na miundombinu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane itaendelea kutunga sera na sheria pamoja na kubuni mipango yenye lengo la kuimarisha ustawi wa wazee na kuhimili ipasavyo ongezeko lao ndani ya nchi na katika famili, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) alipokuwa akitoa hutuba yake katika Mkutano wa mwaka wa mapitio ya wadau ya programu ya uwajibikaji na utekelezaji wa huduma za kinga jamii kwa Wazee (AFFORD) uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano Hoteli ya Verde,Mtoni Zanzibar. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 18, 2021 wakati akifungua semina ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mradi wa Uwajibikaji na Utimilifu kwa Wazee (Afford II) kwa kipindi cha mwaka 2020 na Mpango wa mwaka 2021, semina iliyofanyika katika Hoteli ya Verde, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Serikali itazingatia mahitaji ya wazee katika ujenzi wa miundombinu, maakazi, pamoja na sekta ya afya.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kuimarisha ushirikiano ili kuona kwamba jitihada za kuwatunza wazee zinaleta ufanisi mkubwa zaidi unaokusudiwa.

Amesema kuwa, tayari kuna Sheria ya Masuala ya Wazee Namba 2 ya mwaka 2020 ambayo imeweka utaratibu wa upatikanaji wa haki na huduma za ustawi kwa wazee, ikiwemo urasimishaji wa Mpango wa Pensheni jamii na usimamizi wake.

Ameongeza kuwa, hatua inayofuata hivi sasa ni kuhakikisha uundwaji wa kanuni za sheria hiyo ili iweze kutumika rasmi na kuiagiza Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar iharakishe hatua za kukamilisha kanuni hizo kwa kushirikiana na taasisi husika.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, miongoni mwa mambo atakayoyapa msukumo zaidi katika kipindi chake cha uongozi ni pamoja na kuhakikisha kwamba kinga jamii kwa wazee inaimarishwa.

Amesema kwamba, Serikali itaendelea kuimarisha afya za wazee nchini kwa kuhakikisha kuwa wazee wanaendelea kupata huduma stahiki zikiwemo, huduma za afya bure pamoja na kutambuliwa na kupewa vitambulisho.

Rais Dkt. Mwinyi amekubali ushauri wa wazee wa kuwekwa sehemu maalum kwa ajili yao kwa kupata kipaumbele cha kuhudumiwa wanapofika hospitalini kama walivyomuomba Januari 7, 2021 alipokutana nao Ikulu jijini Zanzibar.

Pia, mtaalamu kuhusu magonjwa yanayowasibu wazee yaani “geriatrics medicine” sambamba na kuongeza wataalamu wa afya waliobeba kwenye taaluma hiyo.

Akizungumza juu ya kuongeza kiwango cha fedha na kupunguza umri wa kuanza kupata pensheni kuanzia miaka 65, Dkt. Mwinyi alisema kuwa, amepokea maombi hayo na ameahidi kuyatekeleza pale hali ya kiuchumi itakapoimarika.

Amesema kwamba, Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha kinga jamii inapewa umuhimu katika mikakati ya kitaifa ambapo katika mpango wa miaka mitano, Zanzibar inaahidi kuendelea kurekebisha na kuimarisha mfumo wake wa kinga jamii kwa makundi yote.

Amesema kwamba suala la kuwajali na kuwaenzi wazee kivitendo hapa Zanzibar ni la kihistoria ambapo licha ya kwamba mila na sila zinafunza hivyo, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea Awamu ya Kwanza, mara tu baada ya Mapinduzi 1964 ilianza mfumo wa kuwahifadhi wazee kwa kuwapatia huduma za msingi.

Amesema kuwa, Serikali ilianzisha nyumba za makazi kwa ajili ya wazee katika eneo la Sebleni na Welezo kwa Unguja na Limbani kwa Pemba sambamba na kutekeleza Sera na mipango mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ustawi na katika mwaka wa 2016 ilianzishwa Pensheni Jamii.

Amesema kuwa, kufuatia mpango huo wazee wote wenye umri kuanzia miaka 70 na kuendelea wamekuwa wakipewa pensheni kila mwezi tangu mwaka 2016 ambapo Pensheni Jamii ilizinduliwa na kuaza kazi rasmi.

Ameongeza kuwa, mpango huo unagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na unagharimu bilioni 6.9 kila mwaka ambapo hadi kufikia Disemba 2020 jumla ya wazee 28,513 kati yao wanaume ni 11,899 na wanawake 16,614 wamepatiwa malipo ya pensheni jamii katika Shehia zote za Unguja na Pemba.

Kaimu Waziri wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Simai Mohamed Said alisema kuwa, maamuzi ya kufanyika mkutano huo hapa Zanzibar hayakuja kwa bahati nasibu isipokuwa ni kutokana na hadhi kubwa iliyonayo Zanzibar duniani katika kuwajali, kuwaenzi na kuwaheshimu wazee.

Nae Naibu Balozi wa Ireland nchini, Chloe Horne amesema kuwa, Ireland kupitia Shirika lake la “Irish Aid’ imekuwa ikiunga mkono juhudi hizo kwa muda mrefu huku akisifu juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajali wazee hasa katika kuanzisha Pensheni Jamii.

Amesisitiza kwamba, nchi yake itaendelea kuratibu miradi hiyo kwa Tanzania pamoja na nchi nyingine zikiwemo Malawi, Msumbiji na Ethiopia ambazo wamekuwa wakiziunga mkono kwa miaka kumi hivi sasa.

Mapema Mkurugenzi wa “Help Age International”, Smart Daniel amesema kuwa, hivi sasa dunia ina wazee milioni 901 sawa na asilimia 12 ya watu wote duniani idadi ambayo ni kubwa kuliko watoto walio chini ya umri wa miaka 5, idadi ambayo ifikapo mwaka 2050 kutakuwa na wazee bilioni 2.92 sawa na asilimia 21 ya watu wote duniani ambapo wazee watakuwa wengi kuliko watoto wote wenye umri wa miaka mitano.

Amesema kuwa, ongezeko hilo linatoa msukumo kwa dunia kutoa sera bora zaidi za kuwahudumia wazee ili kuwafanya waendelee kutoa mchango wao wa kutukuka kwa maendeleo ya jamii zao na dunia kwa jumla.

Mkurugenzi huyo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha na kuendelea kutoa Pensheni Jamii kwa wazee wote wenye umri wa miaka 70 na kuendelea na kusema kuwa jambo ambalo limeiletea nchi sifa kubwa ya jinsi Serikali inavyothamini wazee na kuiwezesha pia kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine.

Amesema kuwa, mfano mzuri uliooneshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Pensheni Jamii kwa wazee wote imewatia mataifa mengine moyo wa kuanza kutoa pensheni kwa wazee wao na kutolea mfano nchi jirani za Kenya na sasa Uganda ambazo tayari wameanza kutoa Pensheni kwa wazee.

Amempongeza mafanikio ya SMZ ya kutunga Sheria ya kusimamia mambo ya wazee ikiwemo Pensheni Jamii kwa wazee wote ambayo tayari imeshasainiwa na kueleza iwapo kanuni zikikamishwa kuiwezesha sheria hiyo kutumika rasmi itaimarisha sana maisha ya wazee.

Katika semina hiyo Salum Mohamed amewasilisha mada juu ya Mifumo ya Ulinzi wa Jamii barani Afrika kwa kupitia mifano ya mfumo wa Kinga Jamii Zanzibar. 

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, dini na serikali walihudhuria katika semina hiyo yakiwemo pia, makundi ya wazee, washiriki kutoka nchi za Ethiopia, Msumbiji na Malawi na wengineo.

Mara baada ya kupokelewa katika viwanja vya hoteli hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alipata kuona burudani ya ngoma ya asili ya Kibati. 

Post a Comment

0 Comments