Bei ya pamba yapanda, Serikali yatoa maelekezo kwa wakulima

Serikali imetangaza rasmi bei ya zao la pamba katika msimu mpya wa ununuzi wa zao hilo mwaka huu msimu wa 2020/21, ambapo kilo moja itanunuliwa kwa Shilingi 1,050 kwa pamba daraja la kwanza, huku daraja la pili bei yake ikiwa Shilingi 525, anaripoti Derick Milton (Busega).
Bei hiyo mpya iliyotangazwa leo ni ongezekezo la Shilingi 240 ya Bei iliyotangazwa mwaka jana msimu wa 2019/20 ambapo ilikuwa Shilingi 810 kwa kilo moja sawa na asilimia 30 ya ongezeko la bei hiyo iliyotangazwa leo.

Akitangaza bei hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera kwenye hafla ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa zao hilo iliyofanyika katika kijiji cha Mkula amesema kuwa, licha ya bei kupanda bado tija imekuwa ndogo kwenye zao hilo.

Mwera amesema kuwa, katika msimu wa mwaka huu, uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 122,650 msimu wa mwaka 2019/20 na kufikia tani 393,000 msimu wa 2020/21 ongezekezo la asilimia 68 ya uzalishaji, ambapo mkoa wa Simiyu umezalisha tani 141,095

Aidha, amesema kuwa bado Kuna changamoto ya wakulima kufuata Kanuni Bora za kilimo ili kuzalisha kwa tija, ambapo asilimia 30 ya wakulima wote wa zao hilo wameendelea kutofuata kanuni hizo na kulima kienyeji na kutaka wadau wote wa pamba kuendelea kutoa elimu ili wakulima wote wazalishe kwa tija.
"Niagize halmashauri pamoja na bodi ya pamba, kuhakikisha Elimu zaidi inawafikia wakulima kufuata kanuni bora za kilimo, lakini pia kuimarishwa shughuli za ugani kwa maafisa ugani kwa kuwapatia vitendea kazi ikiwemo usafiri ili waweze kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwapa Elimu," amesema Mwera.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameitaka bodi ya pamba kushirikiana Mahakama, katika kuanzisha Mahakama inayotembea kuweza kuwachukulia hatua kali wale wote ambao watabainika kuchezea mizani ya kupitia kwa lengo la kuwaibia wakulima.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi wa Bodi ya pamba Marko Mtunga amesema kuwa licha ya serikali kutoa Elimu kwa wakulima kufuata kanuni bora za kilimo, bado eneo la kupanda kwa mstari limekuwa changamoto kubwa kwa wakulima.

"Tija inapotea ana kwenye eneo hili la kupanda kwa mstari, ingawa baadhi wanafuata kanuni hii lakini wengi bado hawafuati kanuni hii na kisababisha tija kuendelea kuwa kidogo, kuna mkulima anaweza kulima shamba la hekari 10 lakini mavuno yake ni shamba la hekari tatu kwa sababu hajafuata kanuni," amesema Mtunga.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewataka wadau wa zao hilo kuhasisha wakulima kujiunga na Amcos kwani changamoto nyingi ambazo zinalikabili zao hilo utatuzi wake upo chini ya Amcos ikiwa wakulima wengi watajiunga

Joshua Emmanuel mmoja wa wakulima ameishukuru bei kuongezeka huku akieleza kuwa bado ongezekezo hilo halijaleta matumaini kwa wakulima walio wengi kutokana na kutumia gharama kubwa katika uzalishaji.

Naye Katibu wa Chama cha wanunuzi wa pamba nchini Boaz Ogolla amesema kuwa wanunuzi wako tayari kununua pamba yote ambayo wamezalisha wakulima kwani uwezo upo na uhitaji ni mkubwa kwenye viwanda vyao.

Hata hivyo licha ya serikali kutangaza bei, lakini haikutangaza mfumo upi wa ulipaji wakulima utatumika kama utakuwa wa benki, simu au pesa taslimu kama ambavyo ilitangazwa uko nyuma kuwa mfumo utakaotumika msimu huu ni Benki na simu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news