KAMISHNA YAMBESI AWATAKA WATUMISHI WA KADCO KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa George Yambesi amewataka Watumishi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (KADCO) kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, ANARIPOTI MWANDISHI MAALUM TUME YA UTUMISHI WA UMMA (Kilimanjaro).

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (katikati) akisisitiza jambo kwa watumishi wa KADCO (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo yanayotolewa na Tume ya kuwajengea uwezo, kulia ni Dkt. Natu Mwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kilimajaro na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO, Bibi Christine Mwakatobe (kushoto). (Picha na PSC).

Mheshimiwa Yambesi amesema haya leo Mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa KADCO kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na usimamizi wa Utendaji Kazi kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS) yaliyoandaliwa na KADCO na yanatolewa na wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma.

Alisema, watumishi wa KADCO wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma kwa kufanya kilicho sahihi huku wakizingatia utaalamu, uaminifu na uwajibikaji katika utendaji kazi wao wa kila siku wakati wa utoaji huduma.

“Naipongeza Menejimenti ya KADCO kwa kuandaa mafunzo haya kwa Watumishi ambayo naamini yataboresha utendaji kazi wenu na uzingatiaji wa Sheria wakati wa ushughulikiaji wa haki na wajibu wenu na wa wengine wakati wa utoaji wa huduma katika uwanja wetu wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA). Ni muhimu wakati wote mkafahamu kuwa nyinyi ni Taasisi ya kibiashara, wakati wote mnatakiwa kwa mbele kiushindani ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ” amesema.

Mheshimiwa Yambesi amesema kuwa hakuna Haki isiyo na Wajibu, Waajiri wana wajibu wa kuhakikisha watumishi wa umma wanapata stahili zao zote za kiutumishi ambazo ni haki yao kwa wakati na watumishi wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ambayo ni haki ya Waajiri.

“Hivyo, ni muhimu kwa watumishi wa umma kupandishwa vyeo, kuthibitishwa kazini na kulipwa stahili zao mbalimbali kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Aidha, Watumishi wa Umma wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu, uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kupata stahili zao,”amesema.

Kamishna Yambesi amesema miongoni mwa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma ni pamoja na kutoa Miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma; Kupokea na kushughulikia rufaa za mashauri yaliyotolewa maamuzi na Mamlaka za Nidhamu; Kuwezesha, kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa Umma wa ngazi mbalimbali ili uwe wa ufanisi na wenye kuzingatia matokeo.

Akizungumzia kuhusu OPRAS Mheshimiwa Yambesi amesema OPRAS ipo kisheria ni vizuri watumishi wa KADCO na watumishi wa umma wakaielewa vizuri ili kila mtumishi aweze kupimwa utendaji wake na apate anachostahili kwa haki bila upendeleo na upandishwaji cheo kwa mtumishi kutokane na ufanisi wake katika utendaji wa kazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (KADCO) Dkt. Natu Mwamba amesema mafunzo haya yanafanyika kipindi ambacho KADCO inaandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano ijayo ni imani kubwa kuwa malengo ya Tasisi yatakayowekwa yatakuwa ni yenye kutekelezeka na mtiririko wake utakwenda vizuri hadi kwa wafanyakazi ili waweze kuweka malengo yanayopimika katika utendaji kazi wao.


Watumishi wa KADCO wanaoshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo wakiwa na wawezeshaji kutoka Tume ya Utumishi wa Umma wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (hayupo pichani) leo katika ukumbi wa mikutano wa KADCO Kilimanjaro. (Picha na PSC.)

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha mheshimiwa Yambesi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO, Bibi Christine Mwakatobe amesema anaishukuru Tume ya Utumishi wa Umma kwa kukubali kuja kutoa mafunzo haya. Mafunzo haya yanafanyika baada ya Tume kufanya ukaguzi wa masuala ya Rasilimali watu KADCO na kubaini uwepo wa baadhi ya mapungufu. 

 
Menejimenti ya KADCO inatarajia mafunzo haya yatakuwa ni yenye tija na yataongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Amesema jumla ya watumishi 291 wanatarajia kushiriki katika mafunzo haya ya wiki mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news