Rais Dkt.Mwinyi aungana na viongozi wa Dunia mtandaoni kujadili njia za kuimarisha umoja, mshikamano

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, imekuwa ikifanya kazi na mataifa mbalimbali duniani katika kudumisha amani pamoja na kutafuta suluhu ya migogoro kadhaa na kuimarisha usalama na maendeleo, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika mkutano huo kwa njia ya mtandao leo. (Picha na Ikulu).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo leo katika hotuba yake wakati alipoungana na viongozi kadhaa duniani kwa njia ya mtandao katika kujadili njia bora za kuimarisha umoja na mshikamano ambapo mada kuu ilikuwa ni “Kuimarisha umoja kwa kuleta na kudumisha amani hasa katika Rasi ya Korea (Korea Peninsula).

Mjadala huo ambao umefanyika kwa njia ya mtandao kutokana na uwepo wa maradhi ya COVID 19 duniani, Rais Dkt. Mwinyi alianza kwa kumpongeza Dkt. Hak Jan Han mwanzilishi wa Taasisi ya “Universal Peace Federation” kwa kumpa fursa hiyo ya kuungana na viongozi kadhaa duniani katika mjadala huo.

Katika mjadala huo ambapo miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa ni kuwataka viongozi wa Dunia siyo tu kuzungumiza matatizo ya kuzuka kwa maradhi ya COVID 19, bali pia, kuwa na fikra mpya za kuondokana na matatizo yaliyopo na badala yake kuwa wamoja katika hali ya usalama na amani duniani.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa ingawa kijiografia Rasi ya Korea inaonekana iko mbali na Afrika, lakini ikumbukwe kwamba licha ya umbali huo, Afrika imekuwa ikishiriki kikamilifu katika kurejesha hali ya amani na demokrasia katika eneo hilo.

Amesema kuwa, kwa bahati mbaya, licha ya juhudi zilizochukuliwa na Jumuiya za Kimataifa, hadi leo eneo hilo bado limebaki na mivutano ambayo inatishia usalama katika eneo la Kusini Mashariki ya Bara la Asia na kutoa changamoto kadhaa kwa usalama wa dunia kwa jumla.

“Hatuwezi kuendelea kubaki tunautizama tu mgogoro huo, ambapo baadhi ya wakati unajulikana kuwa ni ‘mgogoro uliosahauliwa ambapo kuwepo kwa mgogoro huu kuna athari nyingi kwa amani na usalama wa dunia,”amesema Dkt. Mwinyi.

Kwa msingi huo, Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi kwa Dkt. Han Ja Han, kwa kukusanya timu ya wataalamu kutoka pande mbalimbali za dunia ili waje na rai na fikra mpya zenye lengo la kurejesha hali ya amani na usalama ili kuwa na Korea iliyoungana.

Akizungumzia hali ya kisiasa ya Zanzibar na historia yake, Rais Dkt. Mwinyi amempongeza marehemu Seif Sharif Hamad, kwa kukubali kuungana naye katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo matokeo ya Uchaguzi mkuu yalimuezesha kumteau kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Ameeleza alivyofarijika kwa uamuzi huo wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo ni miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoyapata ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano atakachokuwepo madarakani.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, lengo lake ni kuona kuwa kuna Zanzibar ambayo watu wake ni wamoja na inapiga hatua za haraka za maendeleo.

Amesema, jinsi anavyoamini kuwa hali ya amani na utulivu ndiyo chachu ya maendeleo ya Zanzibar na anahisi hivi sasa Zanzibar imepiga hatua katika kusahau tofauti zilizokuwepo na kuondoa changamoto zilizokuwa zinakwaza maendeleo.

Amesisitiza kwamba, Zanzibar imedhamiria kutumia vizuri rasilimali zake na fursa iliyopo kijiografia ya kwamba Zanzibar iko eneo zuri, eneo la kimikakati na muhimu katika kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi.

Amesema kuwa, Serikali anayoiongoza imejizatiti kuimarisha na kukuza fursa za uwekezaji na kutoa upendeleo maalumu kwa wawekezaji wanaowekeza Kisiwa cha Pemba ili kukuza maendeleo katika kisiwa hicho na kuleta uwiano wa kasi na hali ya maendeleo baina ya Kisiwa cha Unguja na Kisiwa cha Pemba.

“Kuhusu dhamira na malengo yangu niliyonayopanga kuyatekeleza kwa Zanzibar baada ya uchaguzi kwa ufupi, naweza kusema kwamba ni kuendeleza uchumi wa buluu kwa kushirikiana kwa karibu sana na sekta binafsi ili kuweza kufikia malengo yangu ya kuifanya Zanzibar kuwa ni kitovu cha biashara katika ukanda wa Bahari ya Hindi,”amesema Dkt.Mwinyi.

Aidha, amesema kuwa Zanzibar ina fursa na rasilimali nyingi za kuweza kuendeleza uchumi imara utakaoweza kukuza ajira, kupunguza umasikini na hatimae kupata maendeleo ya haraka.

Ameongeza kuwa, Zanzibar imedhamiria kuendeleza uchumi wa buluu kwa kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA) ambazo nazo kwa upande wao zimepanga kuendeleza uchumi huo.

Amesisitiza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar itafaidika sana kwa kuimarisha ushirikiano na nchi hizo katika kuendeleza uchumi wa buluu.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kwamba Serikali anayoiongoza itahakikisha kwamba katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo inashirikiana na Washirika wa maendeleo ili kuweza kufikia malengo yake ya kukuza ajira, kuimarisha sekta ya elimu, afya, na miundombinu kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050.

Rais Dkt. Mwinyi amemuunga mkono Dkt. Hak Jan Han, pamoja na wanachama na marafiki wote wa taasisi ya “Universal Peace Federation” na jumuiya zake katika kuimarisha amani na kuharakisha maendeleo.

Post a Comment

0 Comments