Serikali yaanza kutekeleza maagizo ya kikao cha Rais Samia na IMF

Na Farida Ramadhan, WFM-Dodoma

Serikali imeanza utekelezaji wa maelekezo ya kikao cha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Kimataifa (IMF), Bi. Kristalina Georgieva kilichofanyika kwa njia ya mtandao mwanzoni mwa mwezi huu ambacho pamoja na mambo mengine walijadili kuhusu atheri za kiuchumu na kijamii zilizotokana na changamoto za janga korona (Covid- 19).
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa kikao na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha Kimataifa (IMF) nchini, Bw. Jens Reinke (hayupo pichani) kilichofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia)akimsikiliza Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha Kimataifa (IMF) nchini, Bw. Jens Reinke (kushoto) katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini, Bw. Jens Reinke katika ofisi za Wizara hiyo.

Alisema wamekutana ili kutafsiri maelekezo hayo katika utekelezaji ili kuiwezesha IMF kushirikiana na Tanzania katika kujenga uchumi ambao umekumbana na misukosuko inayoendelea duniani inayotokana na changamoto za janga la korona (Covid- 19).

“Tumekutana na IMF pamoja na Wataalam wa Wizara pamoja na baadhi ya taasisi zake kujadili namna ya kuandaa taarifa ya maeneo yaliyoathirika zaidi na misukosuko hiyo pamoja na kuangalia kiwango cha athari katika maeneo husika”, alisema Dkt. Nchemba.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha Kimataifa (IMF) nchini, Bw. Jens Reinke akizungumza kuhusu namna shirika hilo litachangia kuinua uchumi wa nchi wakati wa kikao na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kilichofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa kikao na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kilichofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Nchemba alisema athari za misukosuko hiyo ya uchumi zinatofautiana kisekta kwa kuwa kuna sekta ambazo zimeathirika moja kwa moja kama biashara, utalii na makusanyo, na kuna zile ambazo haziathiriki moja kwa moja.

Alisema wataangalia athari za misukusuko hiyo katika huduma za jamii kwa upana wake kama huduma za Afya hususani kuboresha miundombinu, dawa na upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na suala la upatikanaji wa maji.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini, Bw. Jens Reinke alisema shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Tanzania na kubainisha kuwa yeye binafsi yupo tayari kufanya kazi na wataalam wa Tanzania ili kusaidia nchi na kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi kama ilivyopangwa.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Maendeleo na Biashara Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo kuhusu namna bora ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Maendeleo na Biashara Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo akizungumzia utayari wa benki hiyo wa kufadhili miundombinu nchini, katika kikao cha benki hiyo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Amina Khamis Shaaban wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), baada ya kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Maendeleo na Biashara Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo baada ya kikao kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango).

Mhe. Dkt. Nchemba alisema Serikali itaufanyia kazi ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na benki hiyo ili kuhakikisha kuwa miradi yote inayofadhiliwa inatekelezwa kwa haraka kama ilivyopangwa.

“Benki ya Maendeleo ya Afrika ni miongoni mwa benki ambazo zinatoa fedha nyingi katika hudumia miradi nchini hususan miradi ya miundombinu, na kesho Mwakilishi wa Benki na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha watasaini mkataba kule Dar es Salaam kwa ajili ya miradi”, alibainisha Dkt. Nchemba.

Alisema kwasasa benki hiyo inafadhili miradi ya miundombinu takribani 22 ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko mkoani Dodoma na mradi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.

Afafanua kuwa Serikali inangojea utekelezaji wa benki hiyo kuwezesha Tanzania kunufaika zaidi na madirisha ya mikopo inayotolewa ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Maendeleo na Biashara Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali.

Alisema benki hiyo iko tayari kuyafanyia kazi mambo yote muhimu waliyojadili ikiwa ni pamoja na kuwezesha Tanzania kunufaika zaidi na madirisha ya mikopo inayotolewa.

Aidha, Bi. Nwabufo alimpongenza Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kupata nafasi hiyo na kutoa salam za pole kutokana na msiba mzito ulioikumba nchi kwa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news