Waliokuwa vigogo wa MSD waachiwa huru

Leo Mei 13, 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu na mwenzake, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha hati mahakamani hapo ya kutokuwa na nia ya kundelea na mashtaka dhidi yao, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mbali na Bwanakunu mshtakiwa mwingine ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Logistiki MSD, Byekwaso Tabura, ambao walikuwa wakishtakiwa na mashtaka matano likiwemo la utakatishaji fedha zaidi ya shilingi bilioni moja.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kassian Matembele wa Mahakama hiyo, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon kuieleza Mahakama kuwa DPP ametoa hati hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Sura ya 20 iliyofanyiwa mapitio 2019.

Baada ya Wankyo, kueleza hayo Mahakama imekubaliana na hati hiyo na kuwaachia huru washtakiwa, ambapo kifungo hicho pia hakizuii washtakiwa hao kutokushtakiwa tena.

Awali, Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah akisoma hati ya mashtaka alidai kuwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 maeneo mbalimbali ya jiji na mkoa wa Dar wa Salaam wakiwa watumishi wa umma kwa pamoja walitengeneza genge la uhalifu kwa ajili ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 20, 2019 washtakiwa wote kwa pamoja waliisababishia MSD hasara ya sh. 3,816,727,112.75.

Shtaka la tatu ambalo linamkabili Bwanakunu ni matumizi mabaya ya madaraka ambapo inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2916 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya Keko wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es Salaam kwa makusudi alitumia nafasi yake kulipa kiasi cha sh 3,816,727,112.75 kwa wafanyakazi wa MSD kama nyongeza ya mishahara na posho bila ruhusa ya Katibu Mkuu Utumishi na hivyo kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Katika shtaka la nne washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya tofauti ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja waliruhusu uhifadhi mbaya wa vifaa tiba uliosababisha vifaa hivyo kuharibika hivyo kuisababishia MSD hasara ya sh 85,199,879.65

Shtaka la tano linalowakabili washtakiwa hao ni utakatishaji fedha ambapo inadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya Keko Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar wa Salaam wote kwa pamoja walijipatia fedha sh. 1,603,991,095.37 wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu ambao ni kuongoza genge la uhalifu.

Post a Comment

0 Comments