WANANCHI TUNDURU WATAKIWA KUTUMIA VYEMA UJUZI WA KUKABILIANA NA TEMBO

Na Happiness Shayo -(WMU) Tunduru

Wananchi 20 kutoka vijiji vya Wilaya ya Namtumbo na Tunduru waliopewa mafunzo ya ulinzi wa wanyamapori na namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu kama tembo wametakiwa kuhakikisha wanautumia vizuri ujuzi huo ili kuilinda jamii inayokabiliwa na tatizo la kuvamiwa na tembo.
Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Revocatus Menei akitoa maelekezo ya namna ya kutumia tochi maalum kufukuza tembo kwa baadhi ya wanakijiji cha Jakika Wilaya ya Tunduru katika mafunzo kwa vitendo yaliyofanyika jana kijijini hapo.Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyama waharibifu kama tembo yaliyofanyika katika ukumbi wa Klasta Wilayani Tunduru jana.

“Ndugu zangu ambao mmekuja kwenye haya mafunzo msiende kuyaweka kabatini, muende mkayafanyie kazi na mkatoe elimu kwa wananchi na mtumie mafunzo haya kuwadhibiti wanyama waharibifu,” Mhe. Mtatiro amefafanua.

Aidha, amewaasa wakufunzi hao kuwa wepesi kutoa taarifa za uvamizi wa wanyamapori waharibifu katika makazi ya watu pindi inapotokea.
Mratibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) Kanda ya Kusini, Richard Katombo akionesha namna ya kutumia mizinga ya nyuki kufukuza tembo aliyevamia makazi ya watu, onyesho lililofanyika katika kijiji cha Jakika Wilayani Tunduru jana.“Nimewakamata wenyeviti kadhaa wanaochukua rushwa na kuruhusu ng’ombe kuingia hifadhini, lakini hii haitasaidia isipokuwa tu pale ambapo mtaamua kutoa taarifa kwa watendaji wa vijiji na ofisi ya mkuu wa wilaya mnapoona makundi ya ng’ombe hifadhini” Mhe. Mtatiro amesema.

Mhe. Mtatiro amewaagiza wakufunzi hao kuhakikisha wanawaelimisha wananchi wengine juu ya mbinu mbalimbali walizojifunza za namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu na pia kuzalisha watu wengi kwenye maeneo yao ambao wana weledi wa udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu ili jamii ibaki salama.

Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Dkt. Janemary Ntalwila amesema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika kuelezea njia rafiki za kukabiliana na uvamizi wa tembo.
Mtafiti wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Dkt. Emmanuel Masenga akionesha namna ya kuchanganya pilipili na oili chafu itakayotumika kumfukuza tembo aliyevamia makazi ya watu,onesho lililofanyika kijiji cha Jakika Wilayani Tunduru.
Mtafiti wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Dkt. Emmanuel Masenga akionesha namna ya kutumia fataki kumfukuza tembo aliyevamia makazi ya watu,onesho lililofanyika kijiji cha Jakika Wilayani Tunduru. Wanaoshuhudia ni ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Dkt. Janemary Ntalwila (kushoto) na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Silvanus Okudo (wa pili kutoka kushoto).
Wahitimu wa mafunzo ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyama waharibifu kama tembo wakionyesha wanavijiji kwa vitendo namna ya kutumia honi kuwafukuza tembo katika kijiji cha Jakika Wilayani Tunduru jana. Wa kwanza kulia ni Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Revocatus Menei.

“Njia zitakazotumika ni njia rafiki na za gharama nafuu kwa mfano matumizi ya mabomu ya pilipili , tochi maalum za kufukuzia tembo, fataki, honi, mizinga ya nyuki, uzio wa vitambaa vilivyolowekwa kwenye mchanganyiko wa oili chafu na pilipili,” Dkt. Ntalwila ameongeza.

Dkt. Ntalwila amesisitiza kuwa, njia hizo zikitumika ipasavyo zitasaidia kuboresha maisha ya wananchi kwa kusaidia kuongeza kipato akitolea mfano matumizi ya njia ya mizinga ya nyuki ambayo ina uwezo wa kufukuza tembo na pia kutoa asali, nta na gundi ya nyuki.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Silvanus Okudo amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uvamizi wa tembo.

”Nia ya Serikali ni kuisaidia jamii kupunguza au kuondokana kabisa na tatizo hili la kuvamiwa na wanyama wakali na waharibifu na tunaamini kuwa wakufunzi hawa watajitahidi kuzuia changamoto hiyo kabla haijajitokeza,” amesema Bw. Okudo.
Baadhi ya wanakijiji cha Jakika Wilaya ya Tunduru wakionyesha kwa vitendo namna ya kutengeneza bomu la pilipili linalotumika kumfukuza tembo mara baada ya kupewa mafunzo hayo na Watendaji kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), jana kijijini hapo.
Wananchi waliopewa mafunzo ya kukabiliana na tembo wakionyesha kwa vitendo namna ya kutumia wigo wa pilipili na oili chafu ili kumfukuza tembo aliyevamia makazi ya watu onesho lililofanyika katika kijiji cha Jakika Wilayani Tunduru jana.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Amiri Abeid ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Libangu Wilaya ya Namtumbo amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wanavijiji kuwadhibiti wanyama wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi yao.

“Lengo la mafunzo haya ni kutuwezesha namna ya kuishi na kukabiliana wanyama wakali na waharibifu kama tembo lakini pia kuchukua ujuzi na kwenda kuwafundisha wanavijiji wengine” amesema Bw. Abeid.

Mafunzo ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu yamehudhuriwa na wakufunzi ishirini kutoka vijiji vya Wilaya ya Namtumbo na Tunduru na yameandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAP

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news