Waonywa kuandikisha kaya hewa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini

Uongozi wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, umewaonya na kuwataka watalaamu wake ambao wameteuliwa kutekeleza zoezi la utambuzi wa kaya zitakazoingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya tatu (TASAF III) kipindi cha pili kufuata sheria, vigezo na utaratibu uliowekwa katika zoezi hilo, anaripoti Derick Milton (Meatu).
Meneja ukaguzi wa ndani mfuko wa kunusuru kaya maskini Tasaf, akitoa mafunzo kwa watalaamu wawezeshaji kutoka Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, watakaohusika na utambuzi wa kaya maskini kipindi cha pili.

Watalaamu hao wameonywa endapo watakiuka vigezo hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria, kwani kabla ya kuanza kutekeleza zoezi hilo wanakula kiapo mbele ya mwanasheria lengo likiwa ni kudhibiti uingizwaji wa kaya ambazo hazina vigezo kama ambavyo ilikuwa katika kipindi cha kwanza cha mpango huo.

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt.Joseph Chilonganyi, wakati akifungua mafunzo kwa watalaamu hao ya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini, ambapo katika wilaya hiyo jumla ya kaya 4,000 zinatarajiwa kuandikishwa.

Chilonganyi amesema kuwa, katika utambuzi wa kaya hizo kipindi cha kwanza cha mpango huo, ziliingizwa kaya ambazo siyo maskini, ikiwemo kaya hewa, kaya za viongozi pamoja na kaya za watu wenye uwezo tofauti na maelekezo ya mpango.

Amesema kuwa, uingizwaji wa kaya hizo ulifanywa na wawezeshaji ambao walipewa dhamana ya kutambua na kuandikishwa kaya maskini, hali ambayo ilipelekea serikali kuchukua hatua ya kuwasimamisha waratibu wa Wilaya nchi nzima wa mpango huo ili kufanyika kwa uchunguzi wa jambo hilo.

"Awamu hii hatutavumilia hali hii itokee tena, tunataka kila mmoja atimize wajibu wake, nendeni mkatekeleze zoezi hili kwa kufuata utaratibu uliowekwa, hatutaki kaya hewa, kaya za viongozi, au watu wenye uwezo awamu hii, ikibainika hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika,"amesema Chilonganyi.

"Tuwe waadilifu, tufanye kazi hii kwa haki, kaya zinazohitajika ni zile maskini kweli, lengo la serikali kuleta mpango huu ni kuhakikisha watu wake wanaondokana na umaskini, tunahitaji kaya husika na hakikisheni mnafuata vile vigezo ambavyo vimewekwa,"amesema Dkt. Chilongani.

Awali akiongea kwenye mkutano huo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Fabiana Manoza amewataka watalaamu hao kuwa makini katika utekelezaji wa zoezi hilo, huku akiwatahadharisha kuwa awamu hii hakuna kiongozi ambaye atavumilia kufanyika kwa udanganyifu kwenye uhakiki huo.

"Katika awamu ya kwanza, watu walisimamishwa kazi kwa makosa ambayo yalifanywa na watu wengine, watu walileta kaya ambazo hazistahili, tunawataka mkaepuke hilo, zingatieni maelekezo mnayopewa na siyo kufanya mambo ambayo siyo sahihi,"amesema Manoza.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tasaf, Meneja ukaguzi wa ndani Tasaf makao makuu, Oscar Paul amesema kuwa, katika Wilaya ya Meatu jumla ya vijiji 39 ambavyo havikuwemo katika mpango huo awamu ya kwanza vitaingizwa katika awamu hii ya pili.

Amesema kuwa, katika awamu ya kwanza, Wilaya ya Meatu ilikuwa na kaya za walengwa 3,852 kutoka katika vijiji 69, ambapo kwenye awamu ya pili jumla ya kaya 4000 kutoka katika vijiji 39 vilivyokuwa bado havijaingizwa zitawekwa.

Paul amesema kuwa, katika kipindi cha pili, zaidi ya kaya milioni moja zitaingizwa kwenye mpango huo, huku walengwa wakiwa zadi ya milioni saba nchi nzima ikiwemo Tanzania Bara na visiwani huku huduma za afya zikitarajiwa kuboreshwa zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news