Waziri Mkuu autaka Mkoa wa Mara kuweka mkakati wa kuitangaza Mbuga ya Serengeti

NA MWANDISHI DIRAMAKINI, Mara

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa wa Mara na Watendaji katika Sekta ya Utalii wabadilike na waweke mkakati wa kuitangaza mbuga ya Serengeti ili kuweza kuvutia zaidi watalii na kuitambulisha mbuga hiyo kuwa iko mkoa humo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea katika uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara kwenye ukumbi wa Bishop Rudin uliopo kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mwembeni mjini Musoma, Mei 18, 2021.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhandisi Robert Gabriel na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samweli Kiboye.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inaboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wa nchi na watu na mwongozo huo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuvutia uwekezaji na kuimarisha biashara.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Mei 28, 2021 wakati akizindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa Bishop Rudin uliopo katika viwanja vya Mwembeni mjini Musoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa mkoa huo wahakikishe watendaji, wataalamu na wananchi wanakuwa nyenzo ya kurahisisha kazi ya kuvutia uwekezaji.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hakikisha watendaji wote wa mkoa wanausoma na kuuelewa ipasavyo mwongozo huu. Hakikisha watendaji wako wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uaminifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”.

Waziri Mkuu amesema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji ambazo endapo zitatumika vema, zinaweza kuipaisha nchi kimaendeleo. “…Nitoe wito kwa uongozi mzima wa mkoa uhakikishe unaratibu vilivyo shughuli za uzalishaji hasa wa malighafi, bidhaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya wananchi na mahitaji ya viwanda vya ndani.

Amesema miongoni mwa maeneo ambayo mkoa wa Mara unaweza kunufaika zaidi kwenye uwekezaji kutokana na fursa zilizopo ni kilimo, mifugo na uvuvi. Serikali ilitoa maelekezo yenye lengo la kuboresha sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ili kuzalisha malighafi za kutosha zitakazotumika kwenye viwanda.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara kwenye ukumbi wa Bishop Rudin uliopo kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mwembeni mjini Musoma, Mei 18, 2021.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhandisi Robert Gabriel na kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara, Samweli Kiboye.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Uwekezaji ishirikiane na mkoa ili kuwezesha Kituo cha Uwekezaji cha Kanda (TIC) kilichopo mkoani Mwanza kuanzisha Kituo cha Kutolea Huduma kwa Pamoja (One Stop Centre) ambacho kinapaswa kuwa na rasilimali za kutosha, vifaa na wataalam wote muhimu.

“Watu wote muhimu wanaopaswa kutoa huduma katika kituo wawepo, wakiwemo wataalamu wa Ardhi, Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Vipimo, NEMC, Bodi ya Nyama, Bodi ya Maziwa”.

Pia Waziri Mkuu ameziagiza idara zote za kisekta katika ngazi ya mikoa na wilaya, zishirikiane katika kubuni njia rahisi zitakazosaidia kuondoa urasimu na kurahisisha uwekezaji katika maeneo yao ili kuongeza ajira na vyanzo vya mapato ya Serikali.

“…Viongozi na watendaji wa sekta ya umma, fanyeni vikao na sekta binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ili kujadili na kutatua kero za kibiashara na uwekezaji zinazowakabili kwa wakati”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka mamlaka husika zihakikishe zinaweka mipango ya urasimishaji sekta isiyo rasmi, kurasimisha namba msimbo, kuwapatia wafanyabiashara ndogo ndogo maeneo ya kufanyia biashara na kuongeza kasi ya upimaji ardhi na kasi ya utekelezaji wa anuani za makazi na postikodi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuchochea fursa za kibiashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news