ZEC yatangaza Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka

Na Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza kuwa Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka utafanyika tarehe 14 Agosti, 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Wadi hiyo Ndugu Mlenge Khatib Mlenge.
Akitoa taarifa ya Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka katika Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa Skuli ya Fedha Chwaka Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Mabruki Jabu Makame alisema Tume itafanya uteuzi wa Wagombea kwa ajili ya Uchaguzi huo tarehe 28 Julai, 2021.

Aidha, Mhe. Mabruki alisema Wagombea watakaoteuliwa na Vyama vyao wataanza kuchukua na kurejesha fomu za Uteuzi tarehe 21 Julai mpaka 27 Julai,2021 ambapo kampeni zitaanza tarehe 29 Julai hadi 12 Agosti mwaka huu.

Katika taarifa yake Mheshimiwa Mabruki Jabu alisisitiza kuwa Uchaguzi huo kwa mujibu wa Sheria hautakuwa na Upigaji wa Kura ya Mapema na aliwataka Wananchi, vyama vya Siasa, Wapiga Kura na Wadau wengine wa Uchaguzi kushiriki kuendelea kudumisha Amani wakati wa matayarisho hadi kukamilika kwa Uchaguzi huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali watu, Mipango na Uendeshaji Saaduni Ahmed Khamis alisema Tume imemteua Ndugu Saidi Ramadhan Mgeni Kuwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chwaka akisaidiwa na Ndugu Jaffar Jihad Juma.

Ndugu Saadun alithibitisha kuwa takriban mambo yote muhimu kwa upande wa maandalizi ya kazi ya kuendesha Uchaguzi huo yanakwenda vizuri kwa Mujibu wa ratiba ya utekelezaji iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Ndugu Saadun aliendelea kusema kuwa, Upigaji Kura wa uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka utafanyika katika maeneo na vituo vilivyotumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo Orodha ya Wapiga Kura itabandikwa katika Vituo hivyo siku saba kabla ya siku ya Upigaji Kura ili kuwawezesha Wapiga Kura kufahamu mapema vituo vyao.

Akitoa ufafanuzi wa Kisheria Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Uchaguzi Khamis Issa Khamis alisema kuwa, kwa kuwa Tume imekamilisha Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020 na ina taarifa za Wapiga Kura walioshiriki katika Uchaguzi Mkuu huo, Daftari litakalotumika kwa Uchaguzi Mdogo wa Chwaka litakuwa lile lile lililotumika kwa Uchaguzi Mkuu.

Ndugu Khamis alivitaka vyama vya Siasa kuteua Wagombea wenye sifa za kugombea kwa Mujibu wa Sheria ili kuepuka kuwekewa Pingamizi wakati wa uteuzi wa Wagombea.

Nao wadau wa Uchaguzi wadi hiyo, waliiomba Tume kuendeleza jitihada zaidi ya kutoa elimu ya Wapiga Kura kwa Wananchi wa Vijijini ili kila mmoja apate haki yake ya Msingi kwani wengi wao wanaoishi vijijini hawana utamaduni wa kutumia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya Kijamii.

Hata hivyo, waliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwashirikisha Wadau wa uchaguzi wakati wa kutekeleza majukumu yao na kuiahidi Tume hiyo kushiriki katika Uchaguzi huo kwa salama na Amani kwa kufuata maelekezo yatakayotolea na Tume.

Ilielezwa kuwa, Tume inaendesha Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Chwaka baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa tarehe 25 Machi, 2021 juu ya kuwepo nafasi wazi ya Kiti cha Udiwani wa Wadi hiyo kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Wadi hiyo Bwana Mlenge Khatib Mlenge kilichotokea tarehe 19 Machi, 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news