ACT Wazalendo yamlilia, Profesa Lipumba aanika historia ya Prof.Baregu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Makundi mbalimbali ya watu, taasisi na vyama vya siasa wameendelea kutoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wakiwemo Watanzania kwa kuondokewa na mwanazuoni nguli nchini ambaye pia ni mwanasiasa hodari, Profesa Mwesiga Baregu.

Kwa nyakati tofauti viongozi wa Chama Cha Wananchi (CUF) na Chama cha ACT Wazalendo wamemweleza kwa kina Profesa Baregu.
CUF kimesema kimepokea taarifa ya kifo cha Profesa Mwesiga Baregu kwa mshtuko na huzuni kubwa kwani pamoja na yeye kuwa mwanasiasa na mhadhiri mwandamizi katika vyuo mbalimbali hapa nchini.

Pia marehemu alikuwa ni mwana mageuzi, muumini wa ujenzi wa demokrasia ya kweli akiamini kwa vitendo katika ujenzi wa mifumo ya kitaasisi na utawala bora.

Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF amesema kuwa, pamoja na mambo mengine Profesa Baregu alijitoa kwa dhati katika mageuzi ya Taifa katika kupata katiba mpya inayotokana na maoni ya Watanzania.

Amesema kuwa, mchango wake utakumbukwa akiwa mjumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais Mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete, lakini pia marehemu alishauri na kusimamia upatikanaji wa maoni ya Watanzania kwa nia ya kupata Rasimu ya Katiba iliyokidhi haja na mahitaji ya wakati wa sasa.

Profesa Lipumba amesema kuwa,Taifa limempoteza msomi mzalendo pia Watanzania wamempoteza mtetezi.

Vivyo hivyo wanataaluma wamempoteza mwanamajumui wa Afrika. "Pia wanasiasa tumempoteza mwanamageuzi wa kweli aliyeishi misimamo yake bila kutetereka, "amesema.

Profesa Lipumba amesema kuwa, CUF wanatoa rambirambi na pole zao kwa familia ya Profesa Mwesige Baregu, ndugu, familia ya wana CHADEMA, Watanzania kwa ujumla pamoja na familia ya wanamajumuyi wa Afrika kwa kumpoteza nguli wa siasa na mzalendo wa kweli aliyeamini kuwa taaluma haiwezi kutenganishwa na siasa.

Kwani wanataaluma ndio daraja la kuunganisha tafiti na maendeleo na kufanya siasa iwatumikie wanyonge Watanzania, badala ya wanyonge kuwatumikia wanasiasa.

Profesa Lipumba amesema kuwa,Juni 13, 2021 alipokea kwa masikitiko na huzuni kubwa, taarifa ya kifo cha ndugu yake Profesa Mwesiga Baregu ambaye alikuwa Mwanazuoni mahiri na mwanachama mwandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Profesa Lipumba akizungumzia namna alivyofahamiana na Profesa Baregu amesema, alifahamiana naye vizuri wakati alipokwenda Chuo Kikuu cha Stanford mwanzoni mwa miaka ya 1980 kusomea Shahada ya Uzamili katika Idara ya Sayansi ya Siasa.

Amesema, yeye alikuwa ametangulia kwenye chuo hicho akimalizia kufanya Shahada ya Uzamili katika Maendeleo ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Stanford, kabla ya Prof. Baregu kujiunga na chuo.

Ameongeza kuwa, walianzisha Umoja wa Wanafunzi wa Kiafrika katika chuo hicho walioupa jina la Stanford African Students Association (SASA).

"Nilipendekeza jina hilo kwa maksudi kwa lengo la kusisitiza kuwa SASA ni wakati wa Afrika kuungana na kujikomboa,"amesema.

Profesa Lipumba amesema kuwa, wanafunzi wengi wa Kiafrika Chuo Kikuu cha Stanford walitokea Afrika Magharibi, lakini alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa SASA kwa sababu ya sifa ya Tanzania kuongoza mapambano ya Ukombozi wa Bara la Afrika.

Amesema, baada ya kumaliza kipindi chake, Prof. Baregu alichaguliwa kuwa Rais wa Pili wa SASA na wanachama wa SASA walijadili matatizo ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo mara nyingi walikutana nyumbani kwa Prof. Baregu kufanya mijadala hiyo.

Profesa Lipumba anasema kuwa, Profesa Baregu alikuwa hodari wa kujenga hoja juu ya umuhimu wa nchi za Kiafrika kuungana ili kupambana na ubeberu.

Amesema, wakiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, "miaka 1980 tulishiriki katika mijadala ya mageuzi ya uchumi yaliyokuwa yakifanyika Arts Lecture Theatre wakati mimi nilipendekeza kufanya mabadiliko kuelekea uchumi wa soko, Prof. Baregu alipinga vikali sera hizo kuwa ni za kukumbatia ubeberu, "amesema Profesa Lipumba.

Mbali na CUF, Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kuwa, kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Profesa Mwesiga Baregu

Akitoa salamu za pole Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma,Salim Bimani amesema, Profesa Baregu atakumbukwa kwa mengi.

Amesema, Prof.Baregu alikuwa mwanazuoni mwenye msimamo usioyumba na mwanasiasa mwanataaluma mwenye kutumainiwa, aliyetoa mchango mkubwa katika harakati na mapambano ya ujenzi wa mabadiliko ya kisiasa na kikatiba katika taifa letu.

"Alijitoa na kujitolea bila woga kuongoza mijadala yenye kushawishi na kutoa shinikizo la kutaka Tanzania irejeshe mfumo wa siasa za kiushindani katika miaka ya 1990, harakati zilizozaa matunda ya mfumo wa vyama vingi tulionao leo.

"Tutamkumbuka pia kwa umahiri wake wa ujenzi wa hoja alipokuwa miongoni mwa wajumbe kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba,"amesema.

Amesema kuwa, ACT-Wazalendo wanaimani ya kwamba, kifo cha Prof. Mwesiga Baregu kimeaacha pengo kubwa katika nchi yetu kutokana na umahiri na mchango mkubwa alioutoa.

"Ni kutokana na hali hiyo, tunatoa wito kwa Serikali zetu zote mbili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Taifa kwa ujumla, kutafakari namna bora ya kuwaenzi wataalamu wetu kwa kuheshimu na kuthamini fikra na mawazo yao tukiamini kuwa hao ni hazina muhimu iliyohitaji kutunzwa kwa maslahi mapana ya vizazi vya sasa na vijavyo,"amesema na kuongeza,

"Kufuatia msiba huu, ACT-Wazalendo tunatoa salaam za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu pamoja na wote walioguswa kwa kumpoteza mwanazuoni huyu nguli,"amesema

Hata hivyo, amesema wanatoa pole nyingi kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambako marehemu Profesa Baregu alikuwa mwanachama aliyepata kutumikia katika nafasi na majukumu mbalimbali ikiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho.

Post a Comment

0 Comments