DODOMA KUANZA KUTOA HATIMILIKI ZA ARDHI ZA KIELEKTRONIKI JULAI MOSI 2021

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Ofisi ya Ardhi mkoa wa Dodoma itaanza kutoa Hatimiliki za Ardhi za Kielektroniki kwa wamiliki wa ardhi kuanzia Julai Mosi, 2021.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonga akizungumza wakati wa zoezi la utoaji hati miliki za ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika mitaa ya Miganga na Chinyika Kata ya Mkonze mkoani Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonga wakati wa utoaji hati za ardhi 223 kwa wananchi waliorasimishiwa maeneo yao kwenye mitaa ya Miganga na Chinyika katika kata ya Mkonze mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa Kabonga, kwa sasa ramani zote za mkoa wa Dodoma zipo kwenye mfumo wa kidijitali hivyo ofisi yake itaanza kutoa hati za ardhi za kielektroniki kwa kuwa hati hizo ziko katika nakala laini.

Kwa sasa Wizara ya Ardhi imewekeza, imeboresha na kuongeza matumizi ya mifumo ya kidigitali ambapo tayari Hati za Kielektroniki nchini zimekuwa zikitolewa kwenye manispaa nne za mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Ilala,Temeke, Kinondoni na halmashauri ya manispaa ya ubungo na hati hiyo ni ya kurasa moja.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde akimkabidhi hati mmoja wa wananchi wa mtaa wa Miganga mkoani Dodoma wakati wa zoezi la kukabidhi hati kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika mitaa ya Miganga na Chinyika mkoani Dodoma.

“Ramani zote za dodoma kwa sasa zipo kidigitali na Julai mosi mwaka huu tunaanza kutoa hati za kieleltroni maana hati zote ziko katika nakala laini,"amesema Kabonga.

Aliwataka wakazi wa Dodoma wanaomiliki ardhi kuhakikisha wanapimiwa maeneo yao na kupata hati kwa kuwa gharama za upatikamaji hati sasa imepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma na kusisitiza kuwa lengo la ofisi yake ni wananchi katika jiji la Dodoma kupata hati zao.

Katika kuhakikisha ardhi ya jiji la Dodoma inapangwa, inapimwa na kumilikishwa, Kamishna Kabonga alisema, ofisi yake ilipeleka timu ya wataalamu katika mitaa mbalimbali ikiwemo ya Miganga na Chinyika kwa lengo la kupima maeneo hayo lakini muitikio wa wananchi umekuwa mdogo.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi hati kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika mitaa ya Miganga na Chinyika mkoani Dodoma.

Naye Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde aliyekuwa mgeni rasmi kwenye zoezi la kugawa hati kwa wananchi wa mitaa ya Miganga na Chinyika alilielezea tukio la utoaji hati kwa wananchi waliorasimishiwa makazi kuwa ni tukio la kihistoria kwa kuwa hati zinawafuata wananchi katika maeneo yao badala ya wao kuzifuta.

Alisema, hatua ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika jiji la Dodoma unaofanywa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi unalifanya jiji hilo kupimwa kwa kasi na kupunguza ongezeko la makazi holela, thamani ya ardhi kupanda sambamba na kuondoa migogoro ya ardhi.

“Leo ni furaha mji unapimwa kwa kasi unaondoa uholela, kuongezeka thamani ya ardhi pamoja na kuondoa migogoro, ukipima eneo unatatua changamoto zote na dododma ikipimika na kupangwa vizuri inakuwa sura ya makao makuu,” amesema Mavunde.
Sehemu ya wananchi wa mitaa ya Miganga na Chinyika katika kata ya Mkonze mkoani Dodoma wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wakati wa utoaji hati kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao kwenye mitaa hiyo

Mavunde amewaeleza wananchi wa mitaa ya Miganga na Chinyika kuwa hati waliyopewa inawapa uhakika wa miliki pamoja na hati hiyo kutumika na taasisis za kutoa mikopo kwa wananchi.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa halmashauri ya jiji la Dodoma William Alfayo alisema, kazi ya upangaji na upimaji iliyofanyika kwenye mitaa miwili ya Miganga na Chinyika mkoani Dodoma ni sehemu ya kazi inayofanyika kwenye kata zote za jiji la Dodoma na zoezi hilo linafanyika kwa mujinbu wa mpango kabambe wa jiji la Dodoma 2019 hadi 2039.

” Tusisahau kilimo cha zabibu katika mipango yetu, sisi tunaendelea na upangaji na upimaji wa mashamba ya zabibu katika maeneo ya Mjini na ninatoa wito kwa wana Dodoma kuzingatia uwekezaji katika zao la zabibu ikiwemo uchakataji wa zao hilo," amesema Alfayo

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news