Na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Dar
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Bw. Sylvester Mwakitalu amekutana na kufanya mazungumzo na watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, mapema leo ikiwa ni sehemu ya kukuza Uhusiano na ushirikiano katika utendaji ili kuwezesha kumalizika kwa mrundikano wa mashauri yaliyopo katika Mahakama hiyo.

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Mwakitalu amesema kuwa, changamoto ya maridhiano (Pre Bargaining) ambayo imeonekana kuwa tatizo amehaidi ndani ya wiki moja itashughulikiwa na kufanyiwa kazi ili ufanisi wa kazi uweze kuendelea,ambapo timu ya maalumu ya Serikali ya masuala ya Kisheria itakutana na kuona namna ya kuboresha Sheria ya Maridhiano katika Kesi mbalimbali hususani za Uhujumu Uchumi. 

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Bw. Godfrey Isaya akieleza baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo katika usikilizwaji wa kesi mbalimbali ikiwemo Upelelezi wa Mashauri kuchukua muda mrefu katika Ukumbi wa Mahakama hiyo Jijini Dar es salaam Juni 11,2021.
Kuhusiana na suala la mashauri ambayo awali yalikuwa yanamtaka Mkurugenzi, kutoa kibali cha kuendesha kesi, ili hali anaweza kuwakasimisha utoaji wa vibali hivyo Waendehsa Mashtaka wa Mikoa, Bw. Mwakitalu amesema kuwa yapo Mashauri ambayo kwa mujibu wa sheria anaweza kuwaelekeza Waendesha Mashtaka wa Mikoa kuyashughulia, lakini yapo mengine ambayo yanahitaji kibali chake.
“Kwa sasa Mashauri yote yatakayofikishwa Mahakamani ni yale tu ambayo upelelezi wake umekamilika ikiwa ni mkakati wa Mahakama ya Tanzania kupitia kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Ibrahim Juma wa kutakwa Mashauri yasizidishe Mwaka yakiwa hayajasikiizwa,"amesema Bw.Mwakitalu
Aidha, Bw. Mwakitalu amesema kuwa kwa sasa atahakikisha anasaini Kesi zote zinazohitaji kibali chake ili zianze kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kuondoa mrundikano wa mashauri hayo Mahakamani.

Bw. Mwakitalu ameongeza kwa kusema kuwa kesi inapochukua muda mrefu upelekea mashahidi wengi kupotea na wengine kutoonekana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuhama au vifo, ambapo amewahakikishia watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ushirikiano mkubwa ili kuwezesha ufanikishaji wa kesi na kupunguza mrundikano wake katika Mahakama hiyo.
“Mfano mpaka sasa jumla ya kesi 369 zimekwishapitisha muda wake hali inayochangia uwepo wa malalamiko ya wananchi, hivyo basi mimi niwahakikishie Ofisi yangu na Watendeji wangu hawatakuwa kikwazo kwa hili nikiwa DPP wakati wangu," amesema Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Mwakitalu.
Awali akisoma Risala kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Godfrey Isaya amesema kuwa, mkoa wa Dar es salaam unazo Mahakama za Hakimu Mkazi Nne ambazo ni Hakimu Mkazi Kisutu,Mahakama ya Watoto,Hakimu Mkazi Kivukoni/Kinondoni na Mahakama ya Jiji/Sokoine.
Mwendesha Mashtaka Mkuu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, Wankyo Simon (katikati) akiwa ameketi pamoja na Mahakimu wa Mahakama hiyo wakati wakimskiliza Mkurugenzi wa Mashtaka Sylvester Mwakitalu Juni 11,2021 katika ukumbi wa Mahakama hiyo.
Hakimu Mkazi Isaya amesema kuwa kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Juni 10,2021 Mashauri mbalimbali yameshughulikiwa ambapo kesi 579 zilibaki kwa Mwaka 2020 huku kesi 132 zikipokelewa hadi Mei, kesi 167 zikisikilizwa.
Aidha, Hakimu Isaya amesema kuwa zipo jumla ya kesi 8 ambazo zimechukua muda mrefu kutokana na mashahidi kuwa changamoto katika upatikanaji wake hali ambayo inapelekea kesi hizo kuchukua muda mrefu pasipo kusikilizwa.
Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es salaam, Bi Mkunde Mshanga, akiteta jambo na Mkurugenzi anayesimamia divisheni ya Uendeshaji wa Mashtaka Nchini, Bw. Osward Tibabyekomya.
Hakimu Mkazi Isaya ameongeza kwa kusema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa moja ni Upelelezi wa Mashauri kuchukua muda mrefu na kuchangia mrundikano wa kesi, pili mashauri mengi kuwa ya muda mrefu hii ikisababishwa na kutopatikana kwa mashahidi, mashauri mengi kusubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashataka na hivyo mengi yanachelewa hata kabla ya kibali kutolewa.
Hakimu Mkazi Isaya amehitimisha kwa kusema kuwa, Mashauri mengi ya Nyara za Serikali,Madawa ya kulevya na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) huchukua muda mrefu sana katika upelelezi wake.
Kikao hicho kilichofanyika leo Juni 11, ni Mwendelezo wa kikao cha awali ambacho kilifanyika mwezi Mei tarehe 21, mwaka huu kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Watendaji na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kikiwa na lengo la kutatua changamoto na malalamiko ya mrundikano wa kesi katika Mahakama hiyo.
0 Comments