Herbinder Seth aachiwa huru, akubali kulipa Bilioni 26.9/-

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Herbinder Seth ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL) leo Juni 16, 2021 ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo Jijini Ilala mkoa wa Dar es Salaam.

Uamuzi huo wa Mahakama, ulipokelewa kwa furaha na shangwe na baadhi ya ndugu jamaa na marafiki ambao walizungumza na DIRAMAKINI Blog kando ya mahakama.

Mahakama hiyo imemuachia huru kwa masharti ya kutokutenda makosa yoyote kwa kipindi cha mwaka mmoja na pia amekubali kulipa fidia ya sh.bilioni 26.9 za kitanzania.

Ni baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ambapo hukumu hiyo, imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kuhusiana na unafuu wa adhabu ya mshtakiwa huyo.

Shaidi amesema, Mahakama imemkuta na hatia mshtakiwa baada ya kukiri kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambazo ni Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Amesema, ni wazi kwamba, Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu ameona kuwa, Seth ni mkosaji wa mara ya kwanza na pia amekubali kuingia makubaliano ya kumaliza kesi na DPP ili kufanya jambo hilo liishe kwa njia mwafaka na Serikali ambayo haiumizi pande zote mbili.

Pia,amesema ni wazi kwamba amekubali kulipa fedha nyingi kwa Serikali, kwa hiyo atatakiwa kuzingatia alichokubaliana na DPP cha kulipa fedha hiyo, kwa hiyo anatakiwa kupewa adhabu ambayo itamfanya alipe hicho kiasi.

Amesema kuwa, mshitakiwa amekaa muda mrefu wa kutosha gerezani, "takribani miaka minne ni muda mwingine wa kutosha sana kukaa kwako ndani umeona mengi na umejifunza mengi, kumepita maji mengi kwenye daraja lako. Mahakama inaamua, kwa kuzingatia yote yaliyodaiwa na pande zote mbili, usitende makosa tena na pia utakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia leo,"amesema Hakimu.

Pia mfanyabiashara Seth ameweka hati ya mtambo wa kufua umeme wa IPTL namba 45566 uliopo kiwanja namba 292/2 kilichopo Kunduchi Salasala mkoani Dar es Salaam kama sehemu ya dhamana iwapo atashindwa kulipa fedha hizo.

Pia tayari mshtakiwa Seth ameshalipa kiasi cha sh.milioni 200 za Kitanzania na kiasi kilichobakia anatakiwa kukilipa ndani ya miezi 12 kuanzia leo.

Awali kabla ya hukumu hiyo kusomwa, Wakili Marandu aliiomba Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria na pia mshtakiwa hana rekodi ya makosa ya jinai.

Kwa upande wa Utetezi, mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, ana tatizo la kiafya halafu amekaa mahabusu kwa muda wa zaidi ya miaka minne, kwa hiyo Mahakama itoe adhabu kulingana na muda aliokaa gerezani.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude wakati akimsomea Seth maelekezo ya awali, alidai katika akaunti ya Escrow iliyopo Benki ya Tanzania (BoT) ilikuwa na fedha kwa ajili ya malipo ya umeme.

Alidai, mshtakiwa aliandika maombi BoT ya kuhamisha Dola za Marekani 22,198,544.60 na sh.309,461,300,158.27 kwenda katika akaunti mbili tofauti zilizopo benki ya Stanbic.

Alidai kuwa, BoT ilihamisha fedha hizo ambazo katika uchunguzi zilitakiwa kulipiwa kodi TRA kiasi cha Sh. 26,946,487,420.08.

Awali, Seth alisomewa upya mashtaka yake ambapo sasa ameshtakiwa na kosa moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuondolewa mashtaka mengine 11 ambayo yalikuwa yakimkabili yeye na mshtakiwa mwenzae James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi mwenza wa IPTL.

Katika shtaka hilo jipya inadaiwa katika tarehe tofauti tofauti kati ya Novemba 29,2013 na Januari 2014 huko katika benki ya Stanbic Tawi la Kinondoni na benki ya biashara ya Mkombozi tawi la St.Joseph ndani ya Manispaa ya Ilala kwa sasa Jiji la Ilala mkoani Dar es Salaam mshtakiwa alitenda kosa.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa, siku hiyo kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa alijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola za marekani 22,198,544.60 na sh.309,461,300,158.27. 
 
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 27/2017 ilipoitwa mahakamani hapo kwa makubaliano.

Post a Comment

0 Comments