Jiji la Dodoma lapongezwa kwa kupata hati safi ya ukaguzi Hesabu za Serikali

Na Dennis Gondwe, Dodoma

MWAKILISHI wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Nathalis Linuma amepongeza ushirikiano wa Baraza la Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopelekea kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu za Serikali.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe (katikati), kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru na Naibu Meya, Emmanuel Chibago (kulia) katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kupitia na kujadili taarifa ya hoja za Mthibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali. (Picha na Dennis Gondwe).

Kauli hiyo ameitoa katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupitia na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa hesabu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2020 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Linuma ambae pia ni Katibu Tawala msaidizi anayesimamia Menejimenti ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisema “nilipopitia taarifa hii, nimeona hoja za Halmashauri ya Jiji la Dodoma hazipo vibaya. 

Hoja nyingi siyo za kupelekea kupata hati mbaya. Katika kipindi hicho, Halmashauri ya Jiji la Dodoma pekee ndiyo ilipata hati safi kati ya halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma. Naomba nichukue nafasi hii kulipongeza sana Jiji la Dodoma. Tulipata hati safi yenye msisitizo. Matokeo haya yanatokana na mshikamano mzuri baina ya Baraza la Madiwani na Menejimenti ya halmashauri”.

Aidha, aliwataka madiwani wa halmashauri hiyo kuendelea kusimamia vizuri taratibu za fedha ili kuiepusha halmashauri kupata hati chafu. Aliwakumbusha kuwa wajibu wao wa msingi ni kuwasimamia wataalam ili wazingatie sheria, taratibu na kanuni katika kutekeleza majukumu yao.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alipongeza maoni mazuri ya wajumbe katika kuboresha utendaji kazi wa halmashauri. “Maoni mazuri hayana mwisho, yatusaidie kuifanya kesho yetu iwe bora kuliko leo. Kukosoana kwa kujenga ni maendeleo. Hakulengi sura ya mtu, bali kunalenga tabia. Tuendee hivyo, ili kuwa Makao Makuu ya nchi kiwe kielelezo cha utendaji kazi” alisema Prof. Mwamfupe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa Halmashauri yake ndiyo pekee iliyosalimika na kupata hati safi kati ya halmashauri nane za mkoa wa Dodoma. 

“Sababu kubwa ni kutokana na kufanya kazi kwa uadilifu, nidhamu na kutii maelekezo ya viongozi ambayo waheshimiwa madiwani ndiyo viongozi wenyewe” alisema Mafuru. Aidha, aliahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi kwa lengo la kuhakikisha halmashauri yake inaendelea kupata hati safi.

Akiwasilisha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa hesabu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2020, Mweka Hazina wa jiji hilo, CPA Rahabu Philip alisema kuwa hoja zote zimejibiwa na kuwasilishwa kwa Mkaguzi wa Nje ndani ya siku 21. 

Alisema kuwa taarifa hiyo inaonesha kuwa halmashauri ina jumla ya hoja 63 kwa mwaka 2019/2020. Katika hoja hizo, 29 ni za miaka ya nyuma na 34 ni hoja za mwaka 2019/2020.

Post a Comment

0 Comments