Kanali mstaafu Lubinga awapa neno viongozi wa mashina wa CCM

Na Jacqueline Liana, Lushoto

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga amewataka viongozi wa mashina ya Chama, katika wilaya za Lushoto na Mkinga mkoani Tanga, kuimarisha mashina ya CCM kwa kuongeza wanachama.
Mwenyekiti wa Shina la Ndeme, kijiji cha Ngazi, Ima Salim, akimkabidhi jana Juni 13, mwaka huu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, taarifa ya utendaji wa kazi wa shina hilo. Kanali mstaafu yuko katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Lushoto na Mkinga mkoani Tanga, kuhamasisha uimarishaji wa mashina ya CCM. (Picha na George Charles).

Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kutembelea mashina ya Chama katika wilaya hizo, Lubinga alitoa wito wa mashina kuimarishwa kwa kuongeza idadi ya wanachama, pamoja na kusimamia maendeleo.

Akifafanua alisema kwamba Chama hakiwezi kusonga mbele pasipo mashina kuwa imara.

"Kuongeza idadi ya wanachama wa CCM ni dhamana waliyo nayo viongozi wa Chama katika ngazi zote za uongozi," alisisitiza Lubinga.

Wajibu mwingine wa mashina ya CCM ni kuhakikisha kila kipengele cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 inatekelezwa kwa maendeleo ya kila Mtanzania.

Alisema serikali inapeleka fedha nyingi katika Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi, hivyo CCM kilichounda serikali wanachama wake wanajukumu la kuhakikisha kila senti ya serikali inatumika kwa manufaa ya wananchi.

Aliwataka watumishi wa serikali kutimiza wajibu wao kwa umma kwa kutenda haki kwani kinyume chake ni dhambi.

"Kuwatendea haki watu ni wajibu wa msingi," alisema na kuongeza haki ikikosekana huweza kuzaa vurugu na migogoro pasipo sababu za msingi.

Aliwataka madiwani kuhakikisha fedha za serikali zinatumika inavyostahili ikiwa ni pamoja na kuboresha miradi ya huduma za jamii; afya, elimu, maji na barabara.

Mashina ambayo yametembelewa na Lubinga kuanzia Juni 12 hadi Juni 13, mwaka huu ni yaliyo katika kata za Duga, Mhinduro na Maramba wilayani Mkinga, pamoja na yale ya kata za Mlalo, Lushoto na Soni katika wilaya ya Lushoto.

Post a Comment

0 Comments