Mtoto adaiwa kuchomwa moto ndani ya Hifadhi ya Jamii Isawima

NA MWANDISHI DIRAMAKINI Blog

Hali ya taharuki imetokea katika maeneo mbalimbali yanayozunguka Hifadhi ya Jamii ya Isawima iliyopo Wilaya ya Kaliua Mkoa wa Tabora baada ya kuibuka taarifa za mtoto mdogo kuchomwa moto ndani ya hifadhi.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Safia Jongo.Kamanda huyo licha ya kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo amesisitiza kuwa, uchunguzi unaendelea na mara moja utakapokamilika watatoa taarifa kamili.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza na DIRAMAKINI Blog, wakazi wa wilaya hiyo wamesema kuwa, hilo ni tukio la kusikitishwa hivyo uchunguzi utakapokamilika na watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine wachukuliwe hatua kati za kisheria.

Salome Luhingulanya ambaye ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kaliua mkoani hapa amesema, taarifa za tukio hilo zimewasikitisha kwani hata kama kuna watu wamevamia eneo hilo wangeweza kuondolewa kwa utaratibu unaoeleweka ikiwemo kupewa notisi maalum.

Amesema kuwa, walialikwa kwenye kikao na kupewa taarifa za tukio hilo ila hawakujua undani wake kwa kuwa viongozi wa chama waliombwa watoke nje ili kuipa nafasi Kamati ya Ulinzi na Usalama na Maofisa kutoka Wizara ya Maliasili kujadili suala hilo.

Luhingulanya amesema, kisheria hakuna mtu anayeruhusiwa kujenga makazi au kufanya shughuli zozote katika eneo la hifadhi ila akabainisha kuwa kwa tukio la kuchomwa moto mtoto huyo anaamini mamlaka husika zitafanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika mapema.

Naye Yohana Lulandala mkazi wa wilaya hiyo ameeleza kusikitishwa na taarifa za tukio hilo na kuomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini waliohusika kuchoma nyumba hizo na kupoteza maisha ya mtoto huyo aliyekuwa ndani na hatua za kisheria zichukuliwe pasipo kumwonea aibu mtu yeyote. Endelea kufuatilia DIRAMAKINI Blog, taarifa mpya zitakujia hapa.
Ng’ombe wakiwa katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima wilayani Kaliua kama walivyokutwa hivi karibuni na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Tabora.

Post a Comment

0 Comments