OFISI YA RAIS UTUMISHI YATOA ELIMU YA MASUALA YA KIUTUMISHI KWA MADIWANI ILI KUHIMIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA UMMA

Na Veronica Mwafisi,Dodoma

Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wametoa elimu ya masuala ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Rufiji kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi yake iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake Mhe. Deogratius Ndejembi.

Akizungumzia ujio wa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi hao wa CCM, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mchengerwa amesema kwa kuwa viongozi hao ni wasimamizi wa haki za watumishi na wananchi ni vizuri wakayaelewa vema majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhimiza uwajibikaji na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika maeneo yao ya utawala.

“Nina imani mkitoka hapa mtakuwa ni chachu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kutoka kwa Watumishi wa Umma kwani Serikali imewaajiri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza.
Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao katika Ofisi yake iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea masuala ya kiutumishi na utawala bora kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi ya Rais-UTUMISHI kujifunza masuala ya kiutumishi na utawala bora. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, hivyo amewaomba viongozi hao ambao ni wasimamizi wa haki za watumishi na wananchi katika maeneo yao, wawahimize watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

“Dhamira ya Mhe. Rais ni kuhakikisha haki za msingi za Watumishi wa Umma zinatekelezwa ili kuwajengea ari ya kutoa huduma bora kwa umma,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa elimu ya masuala ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera, Bi. Mwanaamani Mtoo akitoa elimu ya masuala ya Sera na Miongozo mbalimbali ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi Rais-UTUMISHI iliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji na baadhi ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI baada ya kikao na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliofika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa rai kwa viongozi hao kutumia elimu waliyoipata kuhamasisha watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naye Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Rufiji, Bw. Hassan Makoba amesema, wakiwa wasimamizi wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 watawahamasisha Watumishi wa Umma kutimiza wajibu wao ili wananchi wapate huduma bora.

Bw. Makoba ameongeza kuwa, wameona nia ya dhati ya Serikali katika kusimamia upatikanaji wa haki za Watumishi wa Umma hususan upandishwaji vyeo na malipo ya madai yao mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara, hivyo watakuwa ni mabalozi wazuri wa kuelezea nia njema ya serikali ili watumishi wawajibike ipasavyo.

Viongozi hao wamepata elimu kuhusiana na usimamizi wa Sera na Miongozo katika Utumishi wa Umma, utaratibu wa upandishwaji madaraja, taratibu za uhamisho, stahili za watumishi (Madai ya malimbikizo ya mishahara na stahili nyinginezo) Uhamasishaji wa ujumuishwaji wa masuala ya Anuai za Jamii (Jinsia, Ulemavu, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa) pamoja na uzingatiaji wa Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news