Sekta ya Mawasiliano yachochea maendeleo ya sekta zingine nchini

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Faustine Ndugulile amesema , Sekta ya Mawasiliano imetoa mchango mkubwa kuwezesha ukuaji wa sekta nyinginezo za kijamii na kiuchumi ikiwemo mawasiliano bora,utoaji wa huduma za fedha, elimu,afya,kilimo,usafirishaji na utawala, anaripoti DOREEN ALOYCE (Diramakini Blog).
Hayo ameyabainisha jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari nchini uliolenga kujenga kuboresha utoaji wa taarifa za wizara kwa umma kwa kuwapitisha wahariri kwenye utekelezaji wa majukumu na miradi inayotekelezwa na wizara hiyo .

Dkt.Ndugulile amesema kuwa, kwa kutambua nafasi ya Sekta hiyo Serikali imesambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Hadi kufikia makao makuu ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara na kuiunganisha Zanzibar.

"Sekta hii imechangia asilimia 1.79 kwa Bei za mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 1.5 mwaka 2019 na asilimia 8.4 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2019 na kuwa Sekta ya pili inayokuwa kwa Kasi baada ya Sekta ya Ujenzi,"amesema Ndugulile.

Pia amesema, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha laini za simu zinazotumika zimeongezeka kutoka 48,939,530 mwezi julai 2020 Hadi kufikia laini 53,063,085 mwezi April mwaka huu na kwamba Serikali ipo kwenye uboreshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo mpaka Sasa imeunganisha nchi Saba Kati ya nane zinazopakana na Tanzania.

Katika hatua nyingine ameeleza kwamba katika mwaka wa fedha 2021/22 wizara itaanza kutekeleza mradi wa Tanzania ya kidijitali kwa kuhakikisha wanakuza uchumi wa kidijitali ambapo wananchi watafanya biashara zao kupitia mtandao na wakulima kupata ushauri wa kilimo kupitia simu jambo ambalo litasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwingulu Nchemba akiongea katika mkutano huo amesema kuwa, katika uwasilishwaji wa bajeti bungeni wameipa bajeti kubwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka shilingi bilioni 15 ya mwaka jana mpaka kufikia bajeti ya shilingi bilioni 200 lengo likiwa ni kuendelea kuboresha Sekta ya Mawasiliano hasa barabara vijijini.

Pia amesema kuwa, bado kuna vijiji havina barabara wala zahanati hali ambayo endapo mama mjamzito kapatwa na uchungu kunakuwa na changamoto kubwa namna ya kutoka sehemu ya makazi hadi zahanati ilipo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew amesema, Serikali imejipanga kusimamia Sera ya Tehama juu ya kudhibiti uhalifu na matumizi mabaya ya mawasiliano yanayofanyika mitandaoni.

Nao washiriki wa mkutano wamesema kuwa, mkutano huo umekuwa chachu kutokana na elimu waliyoipata huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa wizara hiyo ili kuendelea kukuza Sekta ya Mawasiliano hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments