TUME: Maafisa Utumishi mnao wajibu wa kuwaelimisha Watumishi waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo

Na Tume ya Utumishi wa Umma, Kisarawe

Maafisa Utumishi wamekumbushwa wajibu wao wa kuwaelimisha na kutoa mafunzo kwa watumishi, si kwa watumishi wapya tu bali kwa watumishi wote ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bwana Nyakimura Muhoji (aliyevaa shati katikati) katika picha ya pamoja na Maafisa wa Tume walioshiriki katika kupokea na kusikiliza kero, malalamiko na changamoto za kiutendaji kutoka kwa watumishi wa umma na wadau Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kuanzia Juni 16 hadi Juni 18, 2021 katika kuadhimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2021. (Picha na PSC).

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Nyakimura Muhoji amesema hayo jana wilayani Kisarawe mkoani Pwani katika mahojiano maalum wakati alipokutana na Maafisa wa Tume waliokuwa Kisarawe kupokea, kusikiliza na kutafutia ufumbuzi changamoto za kiutendaji za kiutumishi katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021 inayoendelea kufanyika.

“Maafisa Utumishi kila mmoja mahali pake pa kazi anao wajibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi kuhusu Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo, Nyaraka na Maelekezo halali yanayotolewa. Wana wajibu pia wa kutoa mafunzo na kujielimisha masuala ya kiutumishi si kwa watumishi wapya tu, bali kwa watumishi wote ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri,”amesema.

Bwana Muhoji alisema jukumu la kutoa elimu kwa watumishi wa umma kuhusu masuala ya Kiutumishi ni la Maafisa Utumishi na Wakuu wa Idara za Rasilimali watu katika Taasisi za Umma, hivyo ni muhimu sana kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na watumishi.

“Maafisa Utumishi mnapaswa kukutana kuelimishana nini mnatakiwa kufanya, waelezeni pia watumishi nini wanatakiwa kufanya. Waraka wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya upo, utumieni na ufanyieni kazi. Wanapowafuata watumishi wajibuni kwa lugha ya staha, tumieni lugha nzuri katika kuwahudumia watumishi wenu, msipowashughulikia matatizo yao watumishi kunapelekea malalamiko,” amesema Muhoji.

Akizungumzia kuhusu kusoma nyaraka mbalimbali, Bwana Muhoji amesema kuwa ni muhimu sana Watumishi wa Umma kuzisoma, kuzielewa na kuzitekeleza ipasavyo nyaraka mbalimbali. Alisema, Maafisa utumishi wanapaswa wakati wote wanapotekeleza kazi zao, wakarejea nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Serikali wakati wa kushughulikia masuala ya watumishi.

Alitoa wito kwa Maafisa Utumishi na Viongozi kuwa tayari wakati wote kusikiliza na kuyashughulikia kwa wakati masuala ya kiutumishi yanayowasilishwa na Watumishi wa Umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news