Uamuzi wa DPP wawanasua Wachina sita Kisutu, watimua mbio

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) ameendelea kurejesha tabasamu kwa watuhumiwa mbalimbali, baada ya utekelezaji wa majukumu yake ambayo yamekuwa na faraja huko Mahakamani.
Ungana na MWANDISHI DIRAMAKINI akujuze, ipo hivi; Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo Jijini Ilala, Dar es Salaam imewafutia kesi ya uhujumu uchumi na kuwaachia huru wafanyakazi sita wa kampuni ya meli ya Sinota Shipping Company.

Ni wale waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kukutwa na ndege mmoja aina ya tausi nchini.

Washtakiwa hao ni raia wa China akiwemo Jin Erhao (35), Chengfa Yang (49), Ren Yuangqing (55), Shu Nan (50), Chen Shinguang (45) na Gu Jugen (57) wote wakazi wa mtaa wa Sokoine jijini Ilala mkoani Dar es Salaam.

Uamuzi huo wa Mahakama umeonekana kuwapa nguvu washtakiwa, kwani baada ya kuachiwa walitoka mahakamani huku wakikimbia na kupanda gari kisha kuondoka eneo hilo.

Hakimu Mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu ndiye aliyewafutia Mashtaka baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania( DPP) kuieleza mahakama kuwa, hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili wa Serikali, Kija Luzugana ameieleza mahakama hiyo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Amesema, Hakimu washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama hii na DPP amesema hana nia ya kuendelea na shauri hili.

Aidha, baada ya Wakili huyo kuipa taarifa hiyo mahakama, Hakimu Chaungu amesema washtakiwa wamefutiwa mashtaka yao na kuachiwa huru.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 57/2020, washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu yaliyowafanya wakose dhamana.

Shtaka la kwanza wanadaiwa Agosti 11, 2020 mtaa wa Sokoine kwa pamoja na kwa makusudi walisimamia genge la uhalifu lililopelekea kupatikana kwa ndege huyo mwenye thamani ya shilingi 1,150,000.

Wakati huo huo, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na nyara ya Serikali iliyopatikana kinyume cha sheria ambayo ni ndege huyo.

Hata hivyo, shtaka la tatu, siku na maeneo hayo kwa pamoja washtakiwa hao walikutwa na tausi huyo huku wakijua kuwa kumiliki ndege huyo ni kinyume cha sheria nchini.

Post a Comment

0 Comments