Wabunge wanawake kuhamasisha wananchi kuhusu Sensa

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Watu wenye Ulemavu imewataka wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani wanawake kwenda kuwa mabalozi wa utoaji elimu kwa wananchi na kuhamasisha watanzania kujitokeza kushiriki kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2022, anaripoti DOREEN ALOYCE (Diramakini) Dodoma.
Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na watu Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama katika mafunzo yaliyotolewa kwa Mtandao wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) kuhusu ukokotoaji wa takwimu yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Aidha, amesema mafunzo hayo yaliyotolewa kwa wabunge hao wanawake ni muhimu hasa katika utendaji kazi wao wa kila siku kwani serikali yoyote haiwezi kufanya jambo la maendeleo kama hakuna takwimu sahihi.
"Kila kitu ni takwimu na ndio maana leo tupo hapa kupeana elimu katika kujua tunawezaje kutumia takwimu hizi, lakini pia kujua pato la Taifa likoje na linatafsiriwaje hivyo kama hatutakuwa na takwimu sahihi mambo hayawezi kwenda,"amesema Mhagama.

Awali akizungumza katika mafunzo hayo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa, wabunge wanatakiwa kujua kwa usahihi takwimu ili ikawe rahisi katika mawasilisho yao pindi wanapokuwa bungeni.
Amesema, takwimu ni sawa na damu katika mwili wa binadamu na iwapo ikatokea Mbunge bungeni anahitaji kupatiwa bajeti katika jimbo lake kuongezewa fedha ni lazima ajue takwimu, Mbunge bila kuwa na takwimu sahihi hawezi kupatiwa bajeti hiyo.

"Katika Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Mwaka 2012 imeonekana kwamba akinamama ndio kundi lenye watu wengi, hivyo wanawake ni Taifa kubwa kwa asilimia 51 na ndio maana leo tuko hapa katika kupeana mafuzo ya masuala ya takwimu ili na ninyi mkawe mabalozi wazuri kwa wanawake katika majimbo yenu,"amesema Dkt.Albina .
Hata hivyo, amesema takwimu zinaonesha idadi ya watu nchini Tanzania inakaribia milioni 60 na idadi hiyo inaonesha wanawake ndio wengi hivyo upatikanaji wa takwimu sahihi unahitajika katika suala zima la maendeleo ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news