Watakaoshindwa kukamilisha zoezi la kupandisha watumishi madaraja kuchukuliwa hatua- Prof.Shemdoe

Na Raphael Kilapilo, Dar es Salaam

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe amesema atachukua hatua kwa viongozi watakaoshindwa kusimamia zoezi la ubadilishwaji wa kada na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi wote walio chini ya OR-TAMISEMI, na kuagiza zoezi hilo kukamilika ndani ya siku moja ya ziada.
Profesa Shemdoe alitoa agizo hilo leo Juni 17, 2021 alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo ambapo pamoja na mambo mengine aliwasisitiza wale wote waliopewa dhamana ya kufanikisha suala hilo kukamilisha haraka, ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Sintokuwa tayari nipoteze kazi kwa sababu ya uzembe wa mtu, kila halmashauri inapaswa kukamilisha kazi hiyo ifikapo kesho, nasisitiza kuwa wale ambao bado hawajakamilisha kazi hiyo hadi hivi sasa kuhakikisha wanaliza kabla ya hatua zingine,” alisisitiza Profesa Shemdoe.

Alieleza kuwa hadi kufikia jana Juni 16, 2021 asilimia 80 ya watumishi 239,000 kutoka mamalaka zote za Serikali za Mitaa walikuwa tayari wameshaingizwa katika mfumo huo huku asilimia 20 iliyobaki ikitarajiwa kukamilishwa Juni 16-17, 2020 tayari kwa utekelezaji wa agizo hilo la Rais Samia.

Aidha alizipongeza Halmashuri zote zilizopambana kwa kujitoa usiku na mchana kufanikisha zoezi hilo, na zaidi pongezi hizo akizielekeza kwa uongozi na timu ya maafisa utumishi wa Jiji hilo la Dar es Salaam kwa ufanisi mkubwa wa utekelezaji wa jukumu hilo.

Kwa mujibu wa Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Jiji hilo Bernadetha Mwaikambo, hadi kufikia jana watumishi 2555 kati ya 2625 walikuwa tayari wameshaingizwa katika mfumo huo wa upandishwaji vyeo na kwamba idadi ya watumishi 70 waliosalia kutokuingia kwao kumetokana na changamoto mbalimbali ambazo Katibu Mkuu huyo wa Tamisemi amesema atazifanyia kazi.

Pia Profesa Shemdoe alisema kuwa awali zoezi la utekelezaji wa mfumo huo lilipaswa kukamilika Juni 12, 2021 lakini kutokana na uwepo wa changamoto mbalimbali walifanya mazungumzo na Wizara ya Utumishi, hatua iliyosaidia kuongezewa muda kidogo ili kulikamilisha.

Alitoa msisitizo kwa maafisa hao kuhakikisha wanapaswa kuitumia fursa hiyo ya ziada iliyotolewa ipasavyo ili kukamilisha suala hilo vinginevyo watachukuliwa hatua za kitumishi.


Kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa umma Na 8 ya mwaka 2002, pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 na taratibu za uendeshaji za mwaka 2003, pamoja na miongozo na nyaraka mbalimbali zilizotolewa na Serikali, Mamlaka ya kupandisha vyeo watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa isipokuwa Walimu kwa mujibu wa Kanuni ya D. (f) na (g) ya Kudumu ya mwaka 2009 ni Halmashauri yenyewe.

Post a Comment

0 Comments