Naibu Waziri Dkt.Mabula awashukia wenyeviti wanaouza ardhi Kilosa

Na Munir Shemweta, WANMM KILOSA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu na kutoa onyo kwa wenyeviti wa vijiji wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro wanaojihusisha na kuuza ardhi ya vijiji bila kufuata taratibu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Kata ya Dumila wilayani Kilosa mkoa Morogoro wakati wa mwanzo wa ziara yake ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo tarehe 12 Julai 2021. Wa pili kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja na kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale.

Dkt.Mabula alitoa onyo hilo tarehe Julai 12, 2021 alipozungumza na wananchi wa kata ya Dumila wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro akiwa katika ziara yake ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara katika mkoa huo.

Akiwa mkoani Morogoro hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Dumila wilayani Kilosa kuhusiana na migogoro ya ardhi waliyoieleza kuwa imekuwa ikisababisha kushindwa kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

Dkt.Mabula alisema, migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikisababishwa na wenyeviti wa vijiji hasa katika suala zima la ugawaji ardhi na kusisitiza kuwa, jukumu la kugawa ardhi ya kijiji kwa mujibu wa sheria ni mkutano wa kijiji na siyo mwenyekiti.
Wananchi wa Kata ya Dumila wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya ya Kilosa.

‘’Naomba muelewe kuwa mwenyekiti wa kijiji haruhusiwi kugawa ardhi na yeyote atakayepewa ardhi na mwenyekiti wa kijiji basi ajue imekula kwake’’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi alimuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe kuwapitisha katika sheria ya ardhi ya usimamizi viijiji wenyeviti wa vijiji ili waweze kuielewa na kusimamia vizuri ardhi katika maeneo yao.

“Kasimamieni vizuri vijiji vyenu na mhakikishe ardhi katika maeneo yenu inapangwa, inapimwa na kumilikishwa maana upangaji ardhi katika maeneo yenu utapunguza migogoro ya ardhi,” Alisema Dkt Mabula.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Martine Shigella akisisitiza jambo wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na wananchi wa kata ya Dumila kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela alimhakikishai Naibu Waziri Mabula kuwa atahakikisha sheria za usimamizi wa ardhi katika mkoa wake zinasimamiwa vizuri ili kuhakikisha migogoro ya ardhi katika mkoa huo inapungua au inakoma kabisa.

Awali Dkt Mabula alianza utekelezaji maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya ya Kilosa kwenye ofisi ya Kata ya Dumila wilayani Kilosa na kuhusisha wenyeviti wa vijiji, watendaji wa mitaa, madiwani pamoja na wananchi waliowasilisha malalamiko kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika kikao hicho, wenyeviti wa mitaa wakiongozwa na madiwani walimueleza Naibu Waziri kuwa, migogoro ya ardhi katika maeneo yao inahusisha mipaka kati ya vijiji, kubomolewa kwa baadhi ya nyumba za wananchi, kutopimwa baadhi ya vijiji, wananchi kuzuiwa kuendelea na shughuli za kiuchumi na wanaodaiwa wamiliki halali pamoja na mgogoro ya uvamizi wa maeneo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi wa wilaya ya Kilosa katika kikao cha ndani kilichofanyika ofisi ya kata ya Dumila wilayani Kilosa mkoa Morogoro wakati wa mwanzo wa ziara yake ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo tarehe 12 Julai 2021. Kushoto ni Katibu Tawala mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja. Na wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga.

Akieleza suala la migogoro ya mipaka, Dkt Mabula alisema, suala la kupima mipaka ni la halmashauri kwa kutenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuhakikisha vijiji vinapimwa na kupatiwa vyeti na alitaka utengaji fedha ufanyike kila mwaka.

“Sisi kama Wizara hatuna wajibu wa kupima mipaka ya vijiji, madiwani mtekekeze majukumu yenu kwa kusimamia upimaji vijiji na msipotekekeza kilosa haitakaa itulie na RAS aunde timu yake chini ya usimamizi wa mpima wa mkoa na kuweka kambi vinginevyo hatuwezi kufika,” alisema Dkt.Mabula.
Viongozi wa wilaya ya kilosa mkoani Morogoro wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya ya Kilosa tarehe 12 Julai 2021. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI).

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wtumishi watatu wa wizara hiyo walioshindwa kuripoti katika kituo chao kipya cha kazi kwenye halmashauri ya wilaya ya Kilosa.

‘’Kama mtakumbuka tulifanya maamuzi magumu kwenye mkoa wa Morogoro kwa kuhamisha asilimia 90 ya watumishi wa sekta ya ardhi na wapo watumishi watatu waliopangiwa kufanya kazi hapa Kilosa lakini mpaka sasa hawajaripoti, namuagiza kamishna wa Ardhi awasiliane na Katibu Mkuu ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao,’’ alisema Dkt.Mabula.

Post a Comment

0 Comments