Maagizo ya Rais Samia kwa mawaziri, naibu mawaziri

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na ushauri wa wataalamu katika utendaji kazi pamoja na kuhuisha Sera na Sheria za nchi zilizopitwa na wakati ili ziweze kufanya kazi ipasavyo. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mawaziri na Naibu Mawaziri katika Kikao Kazi kilichofanyika leo tarehe 13 Januari, 2022 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. (Picha na Ikulu). 

Ametoa maagizo hayo leo Januari 13, 2022 katika Kikao Kazi na Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hazina jijini Dodoma. 

Pia Mhe. Rais Samia amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kufanya kazi kwa kuzingatia Mipango ya kitaifa katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo Dira ya Taifa ya 2020-2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22 - 2025/26 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo inabainisha vipaumbele vya Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi. 

Vile vile, Mhe. Rais Samia amezitaka Wizara zifanye kazi kwa ushirikiano, kuwa na uratibu pamoja na kuzingatia utunzaji wa siri za Serikali. 

Mhe. Rais Samia pia amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kufuatilia utendaji wa kazi wa kila Wizara kwa kutoa ripoti na takwimu sahihi na kufanya ufuatiliaji wa Miradi ili ziweze kutoa taswira sahihi ya namna ya kushughulikia na kutatua kero za wananchi. 

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amewataka viongozi hao kutenda haki na kuwa na usawa kwa watumishi walio chini yao, kufuata kanuni na miongozo ya kiserikali katika utendaji kazi na kuwachukulia hatua stahiki watumishi ambao wanabainika kukiuka kanuni na miongozo hiyo. 

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amewaapisha Balozi Mhandisi Aisha Amour kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na Balozi Said Shaib Mussa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait. 

Hafla hiyo ya uapisho imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news