Rais Samia atoa maelekezo kwa viongozi Kagera kuhusu fedha za maendeleo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi mkoani Kagera kusimamia vyema fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa malengo yaliyokusudiwa.Mheshimiwa Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Juni 8, 2022 wakati akizungumza na wananchi wilayani Biharamulo ikiwa ni katika ziara ya siku tatu mkoani Kagera.

Amesema kuwa, fedha nyingi zimekusanywa na zitaendelea kuletwa kwa wananchi hivyo hakuna haja ya kukaa nazo au kuona zinatuna kwenye mifuko bure, hivyo ni vyema viongozi walioaminiwa wasimamie vyema miradi mbali mbali ya maendeleo inayotolewa na serikali kwa malengo husika.
"Kwa maneno ya mkuu wa mkoa,wakuu wa wilaya na wabunge simamieni vyema fedha hizo kwa matumizi lengwa,"amesema Rais Samia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Charles Mbuge amempongeza Rais Samia kwa namna anavyowajali wananchi katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu kuwa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati zote nchini utakamilika kwa wakati na kwa ubora zaidi ili wananchi waendelee kupata huduma ya afya kwa wakati na kwa ubora zaidi.

Waziri Bashungwa amesema kuwa kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais kuwa hataki kuona majengo ya hospitali yaliyomalizika kujengwa kutotumika na kubaki maboma, Ofisi ya Rais- TAMISEMI inaendelea kutekeleza maagizo hayo akisisitiza kuwa ukamilishaji wa majengo ya vituo vya afya unaambatana na ununuzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba pamoja na ajira za watumishi watakaotoa huduma katika vituo hivyo.
“ Mhe. Rais ulituagiza Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuwa hutaki kuona majengo ya hospitali yanabaki kuwa maboma, lakini pia ulituelekeza ujenzi wa Hospitali hizi, Vituo vya Afya na Zahanati lazima ukamilike ili wananchi wapate huduma, nikuhakikishie Mhe. Rais ujenzi wa miundombinu hii itakamilika kwa wakati na ubora zaidi,” amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwekeza fedha kwa ajili ya uboreshwaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya msingi, barabara pamoja na miundombinu ya elimu Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamiro, Bashungwa amesema miundombinu hii inakwenda kuboresha maisha ya wananchi wa Biharamuro na Mkoa wa Kagera kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, Bashungwa amesema kutokana na maelekezo aliyotoa Mheshimiwa Rais kuhusiana na zao la Kahawa ambalo kwa asilimia kubwa linalozalishwa Mkoani Kagera maelekezo hayo yameleta matumani makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo kwakuwa bei ya kahawa imepanda hadi kufikia shilingi 3720 kwa kilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news