Rais Samia: Serikali inakuja na suluhu ya changamoto ya maji

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inakwenda kutekeleza ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda mkoani Morogoro litakalotumika kukusanya maji wakati wa mvua.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuzindua Mradi wa maji Kigamboni ambao unatoa maji lita milioni 70 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa maeneo mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam kwenye hafla iliyofanyika Kigamboni tarehe 11 Novemba, 2022. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Samia amesema hayo leo Novemba 11, 2022 wakati akizundua miradi ya maji Kigamboni, kukabidhi mitambo ya kuchimba visima na ujenzi wa mabwawa pamoja na kukabidhi eneo la ardhi kwa mkandarasi wa mradi wa bwawa la maji la Kidunda.

Aidha, Rais Samia amesema bwawa hilo lenye thamani ya shilingi bilioni 329 litakalojengwa kwa kutumia fedha za ndani litawezesha kuwepo uhakika wa maji kwa kipindi cha mwaka mzima jijini Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani ambayo kwa sasa yanategemea maji ya Mto Ruvu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi mfano wa ufunguo, Waziri wa Maji Jumaa Aweso pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga mara baada ya kuzindua na kugawa magari ya kuchimbia visima virefu na mabwawa sehemu mbalimbali nchini kwenye hafla iliyofanyika Kigamboni jijini Dar es Salaam.(Picha na Ikulu).

Ujenzi wa bwawa hilo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2022 mpaka 2025 ambapo utakapokamilika utachochea kasi ya maendeleo ya viwanda katika mkoa wa Pwani pamoja na Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine, mradi wa maji wa Kigamboni utaimarisha huduma ya maji katika maeneo ya Temeke, Ilala na Kinondoni hivyo kupunguza ukali wa mgao wa maji.

Hali kadhalika, Rais Samia ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inasambaza maji kwa wananchi katika wilaya ya Kigamboni kwa asilimia 100.
Wananchi wa Kigamboni pamoja na maeneo jirani wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Maji Kigamboni ambao unatoa maji lita milioni 70 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Novemba, 2022. (Picha na Ikulu).

Rais Samia ameitaka Wizara ya Maji kutoa elimu kwa wananchi kuacha kuchoma misitu ovyo, kuchepua maji pamoja na kuingiza mifugo hasa wananchi wanaoishi kando ya vyanzo vya maji kwani vitendo hivyo husababisha upungufu wa maji.

Post a Comment

0 Comments