WAZIRI MKUU AWATAKA WATUMISHI MLELE WAHAMIE KWENYE NYUMBA ZA SERIKALI

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza watumishi wa Halmashauri ya wilaya Mlele wahamie mara moja kwenye nyumba 11 zilizokuwa za wajenzi wa barabara ya Inyonga-Mlele na kukabidhiwa kwa Halmashauri hiyo.

Watumishi ambao ameagiza wahamie kwenye nyumba hizo ni Afisa Usalama wa Wilaya (DSO), Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mlele {OCD}, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini {TARURA} Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mlele {DMO} pamoja na watumishi wengine wa hospitali ya wilaya.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Desemba 13, 2022 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi baada ya kujionea mwenyewe kuwa zimetelekezwa na zinaharibika kwa kukosa uangalizi.

“Watumishi wanahangaika hawana makazi, nyumba zimeachwa nyasi zimeota hadi kwenye korido. Watumishi wote wanaopaswa kuhamia katika nyumba hizi baada ya kumaliza mkutano huu kila mmoja aende kwenye yake na ahamie. Mkurugenzi naomba orodha ya majina ya watakaohamia.”

Nyumba hizo 11 zenye ukubwa tofauti kati yake mbili zinauwezo wa kuchukua familia nne kila moja ni za kisasa na zilikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele Novemba 2022 na Wakala wa Barabara Tanzania {TANROADS} baada ya kukamilika kwa mradi wa barabara.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele uweke utaratibu wa kushirikisha wadau wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo kwenye wilaya yao. Pia aliwataka watumishi hao wahakikishe kila kazi wanazozifanya zinakuwa na matokeo chanya kwa jamii.

Awali, Waziri Mkuu alikagua barabara ya lami ya Inyonga-Mapili yenye urefu wa kilomita 11.7 iliyogharimu shilingi bilioni 8.69. Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Inyonga-Ilunde-Kishelo inayokwenda hadi kwenye mpaka wa mkoa wa Katavi na Tabora ikiwa na urefu wa kilomita 96.

Wakizungumza baada ya ukaguzi huo, baadhi ya wakazi wa eneo la Mapili walimshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo kukamilika kwake kutaimarisha huduma za usafiri wa watu na mizigo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news