Hizi hapa bei za mafuta Januari 2023, Petroli yazidi kushuka huku EWURA ikitoa angalizo

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),Mhandisi Modestus Martin Lumato ambapo bei hizo zimeanza kutumika kuanzia usiku wa saa 6:01 wa kuamkia leo Januari 5, 2023.

"Katika mwezi Januari 2023 bei ya mafuta ya rejareja ya Petroli kwa Dar es Salaam imepungua kwa shilingi nane kwa lita, wakati Tanga na Mtwara imeongezeka kwa shilingi 164 kwa lita na shilingi 168 kwa lita, mtawalia, ikilinganishwa na bei za Desemba 2022.

"Pia bei ya Dizeli kwa Dar es Salaam, Tanga na Mtwara imeongezeka kwa shilingi 48, 91 na 135 kwa lita, mtawalia. Bei ya mafuta ya taa kwa Bandari ya Dar es salaam imepungua kwa shilingi 49 kwa lita ukilinganisha na bei zilizopita,"amefafanua Mhandisi Lumato kupitia taarifa hiyo.

Aidha, ameendelea kufafanua kuwa, kuongezeka kwa bei kikomo kunasababishwa na mabadiliko ya bei za mafuta yaliyosafishwa katika Soko la Dunia (FOB), gharama za uagizaji mafuta (premium) na kuongezeka kwa thamani ya dola ya Marekani ukilinganisha na shilingi.

Aidha amesema, tofauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bandari mafuta yanapochukuliwa na gharama ya usafirishaji.

Mhandisi Lumato amefafanua kuwa, katika kutekeleza bei hizi, wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuzingatia mambo kadhaa.

"Mosi, EWURA inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo.

"Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini. Pili, kwa mujibu wa kifungu namba 166 cha Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.

"EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta.

"Tatu,kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (Price cap) au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa (floor price) kama ilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 57 la tarehe 28 Januari 2022.

"Nne,vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta,punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

"Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

"Tano, wauzaji wa mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na Wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

"Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, na pia, risiti hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.

"Sita,wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei inayooneshwa katika Jedwali Na. 1. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakayekiuka AGIZO hili.

"Saba wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei inayooneshwa katika Jedwali Na. 2 isipokuwa kwa wateja wenye msamaha wa kodi. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakayekiuka AGIZO hili,"amefafanua Mhandisi Lumato. TAZAMA BEI HAPA CHINI KATIKA MIJI MBALIMBALI NCHINI;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news