Kwa nini Bima ya Afya kwa Wote ni faraja kwa watu wenye kipato duni hapa nchini?

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema,Serikali ipo tayari kwa ajili ya utekelezaji na usimamizi wa bima ya afya kwa wananchi wote iwapo Bunge litawakubalia na kuupitisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022 mwezi ujao.
Pia amesema, kwa sasa Serikali imefanya maboresho makubwa katika hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za Taifa huku zikitoa huduma za uhakika nchini kote.

Mheshimiwa Waziri Ummy ameyasema hayo Januari 23, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi cha pamoja na wahariri wa vyombo vya habari nchini wakiwemo watumishi mbalimbali wa wizara hiyo.

"Wakati wa Uhuru huduma za afya zilikuwa ni bure, sera ya Serikali ilikuwa ni kutoa huduma za afya bure kwa wananchi.
"Lakini miaka ya 1990 ikabainika kwamba bure haiwezekani. Serikali kupitia Sera ya Afya ya mwaka 1997 ikaanzisha msingi wa wananchi kuchangia huduma za afya, kwa hiyo tukiangalia sera ambayo tunayo mpaka sasa hivi, Sera ya Afya ya Taifa mwaka 1997 inasema kwamba, wananchi watachangia huduma za afya.
 
"Haikusema utaratibu, kwa hiyo kupitia malipo ya kabla au ya papo kwa hapo, lakini pia ikaweka msingi wa msamaha kwa makundi matatu wakiwemo wazee wasio na uwezo, watoto chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito.

"Kwa hiyo, hatua ya kwanza mwaka 1999 ikapitishwa Sheria ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kwa ajili ya watumishi wa umma.

"Baada ya NHIF kuanza kazi, mwanzoni haikupokelewa vizuri kukawa na 'reservation' kutoka kwa vyama vya wafanyakazi, lakini baadae ikaonekana kwamba ni mkombozi katika kutoa huduma za afya kwa watumishi wa umma. Wananchi ambao nao hawako kwenye utumishi rasmi wakataka kujiunga na NHIF, Serikali ikafanya maboresho ya sheria ikasema wanaruhusiwa kujiunga ambao nao pia sio watumishi wa umma.

"Kwa watumishi wa umma sheria ilikuwa kwamba ni lazima kujiunga, lakini kwa hawa wengine wanajiunga kwa hiari...kwa hiyo baada ya kupitisha mchakato wa NHIF 2016, tukaanza mchakato wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote hatukuukamilisha. Na hatukuukamilisha kutokana na ajenda mbili.

"Ya kwanza ni kugharamia makundi yasiyo na uwezo, tunapokwenda kuifanya Bima ya Afya kuwa lazima, je? Serikali iko tayari kugharamia wananchi wasio na uwezo au tunakuja na utaratibu wa aina gani?.
"Suala la pili ilikuwa ni kuendelea kufanya 'actuary study' (tathimini ya uhai) ili tuweze kuona kama hii sheria tunayopendekeza itakuwa na kiwango gani wananchi kuchangia Bima ya Afya, kwa hiyo ilifika mwaka 2019 hatukuweza kukamilisha nikaondoka wizarani, lakini Dkt.Gwajima (aliyekuwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima) akaendelea kupeleka muswada huu mbele, 2021 ukapita katika ngazi za awali ukarudi nyuma 2022, tunashukuru tumefika mpaka bungeni hadi ngazi ya kamati."

'Acturay Study' ni nini?

Hii ni taaluma ya kisayansi inayotathmini hatari za kifedha katika nyanja za bima na fedha, kwa kutumia mbinu za hisabati na takwimu.

Sayansi ya uhalisia hutumia hisabati ya uwezekano na takwimu kufafanua, kuchanganua, na kutatua athari za kifedha za matukio yasiyo na uhakika ya siku zijazo.

"Na kamati imeweza kupitisha kwa hiyo tukaona kuna mambo mawili ya kuwekana sawa, tukauchomoa, lakini nataka kuwahakikishia sasa Serikali ipo tayari kwenda mbele kuwasilisha na kupitisha endapo Bunge litatukubalia," amefafanua Waziri Ummy.

Umuhimu wa bima hii

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu bima hii mkombozi kwa Watanzania wote hususani wenye kipato duni (maskini). Kwani, pasipo kuwa na rasilimali za kutosha ni vigumu kutoa huduma bora za afya, hivyo wakiichangia wengi kupitia bima ya afya kwa wote itarahisisha huduma za matibabu kuwafikia wengi kwa urahisi.

"Kwa Tanzania sasa hivi Bima ya Afya kwa Wote ni muhimu sana. Bima ya afya ni kwa ajili ya kumsaidia Mtanzania hususani maskini, wote ni mashaidi, Mtanzania akipata mgonjwa atauza baiskeli yake, atauza pikipiki yake, atauza shamba lake.

"Tuna kesi nyingi zenye ushaidi Watanzania wanauza nyumba zao ili kuuguza mgonjwa ili kugharamia mgonjwa, kwa hiyo kwetu Serikali kupitia Wizara ya Afya, bima ya afya ni moja ya sehemu ya kumkomboa mwananchi maskini, kwa sababu atapata huduma za matibabu bila kikwazo,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu.

Pia amesema, wamepokea ushauri na maoni ya wadau mbalimbali nchini na wao wamependekeza jedwali la marekebisho. Ikiwemo sababu ya kufungamanisha bima ya afya na huduma nyingine.

Waziri Ummy amesema kuwa, asilimia 15 tu ya Watanzania ndio wamejiunga na kunufaika na bima ya afya ambapo asilimia 99 wamejiunga na bima wakati wakiwa wagonjwa, kitu kinachoondoa dhana ya bima, kwani mtu anatakiwa ajiunge kabla ya kuugua.
"Asilimia 99 ya wanaokata bima NHIF karibu wote ni wagonjwa. Hata Toto Afya Card niliileta kwa nia njema nikiamini watoto hawaumwi, kwa hiyo kuanzia mika mitano hadi saba walikata bima hiyo kwa shilingi 50400.

"Lakini ukweli ni kwamba, mzigo sasa ni mkubwa, matumizi yake ni mara 300 katika kila shilingi 100 aliyojiunga anatumia shilingi 300, ndiyo maana tumesema iwe lazima ili hata wasioumwa waweze kuingia, "amefafanua Mheshimiwa Waziri Ummy.

Pia amesema, ni lazima kuwa na bima ya afya, lakini sio kosa la kisheria kwa kutokuwa nayo na hakuna mtanzania atakamatwa wala kufugwa kwa kuikosa.

“Japo muswada huu unapendekeza kila mtanzania ajiunge na bima ya afya kwa kufungamanisha na baadhi ya huduma za kijamii, lakini hakuna mtu atakayekamatwa kwa kuwa hajajiunga na bima ndio maana Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kila mtanzania kuwa na bima ya afya na kuweza kujiunga ili kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

"Hamna atakayekamatwa, kushtakiwa wala kufungwa kwa kutokuwa na bima ya afya, lakini tunakuambia ukitaka kupata leseni lazima upate bima ya afya.

"Mfano ukiwa Rwanda, ukiwa barabarani na ukikamatwa unaulizwa bima yako ya afya ipo wapi, huku unaulizwa leseni tu, kwa hiyo Rwanda bima ya afya ni lazima hata ukienda ofisi ya halmashauri unataka hati ya eneo lazima uwe na bima ya afya,"amefafanua Mheshimiwa Waziri.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Ummy amesema,Bima ya Afya si jambo rahisi huku akitolea mfano nchini Marekani kuwa, wamejadili suala la hilo kwa miaka zaidi ya miaka 100 na kwa sasa kwao bima ya afya ni lazima kwa kila mtu na ni gharama.

Prof. Makubi

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof.Abel Makubi amesema, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii ili kupata uelewa mpana kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote.
Amesema,ni muhimu kila mwananchi kuwa na bima ya afya kama nyenzo itakayomsaidia kupata matibabu wakati wote bila kujali hali yake ya kipato.

Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa,wizara imeendelea pia kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali na kufanya maboresho katika maeneo ambayo yalionekana yana uhitaji wa kufanyiwa hivyo hususani ufungamanishaji wa huduma, kwani baada ya kupokea maoni baadhi ya maeneo yamepungua kutoka tisa hadi kufikia matano.

Msemaji Mkuu

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Gerson Msigwa ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya faya kwa wote.

Msigwa amesema, vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuweza kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, hivyo wakishiriki kikamilifu kutoa elimu itasaidia kuwapa uelewa ambao utawasaidia kuendelea kujiandaa kidogokidogo kwa ajili ya kupata bima hiyo.
Pia amesema, anaamini bima ya afya kwa wote inakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto za kugharamia matibabu ambazo wananchi wamekuwa wakikumbana nazo mara kwa mara nchini.

TIRA

Naye Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware amesema, mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha inasimamia na kuhakiksha huduma bora za bima ya afya zinatolewa kwa wananchi wote nchini.

Dkt.Saqware amesema, watafanya hivyo kwa kwa mujibu wa sheria na kanuni ili kuwezesha kila mtanzania kunufaika na huduma bora zitakazokuwa zikitolewa katika vituo vyote vya afya.

Konga

Akiwasilisha mada kuhusu Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote katika mkutano huo, kwa niaba ya Kikosi kazi cha Serikali kinachosimamia mchakato huo ambacho kimeundwa na taasisi mbalimbali,Bw.Bernard Konga ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ametaja baadhi ya huduma ambazo wananchi watakazonufaika nazo ikiwemo ada ya kuandikisha na kumuona daktari, gharama za vipimo, dawa na gharama za kulazwa.

Pia amesema, huduma zingine ni gharama za dawa zote kama zilivyoainishwa katika Orodha ya Taifa ya. Dawa Muhimu (NEMLIT), gharama za upasuaji mdogo, mkubwa na ule wa kitaalamu zaidi unaofanywa na madaktari bingwa.

Konga amesema, pia kuna huduma ya afya kinywa na meno, huduma za matibabu ya macho, vifaa saidizi na huduma ya mazoezi ya viungo.
"Huduma zingine atakazonufaika ni gharama za dawa zote kala zilivyoainishwa katika Orodha ya Taifa ya. Dawa Muhimu (NEMLIT), ada ya kuandikisha na kumuona daktari, gharama za vipimo, upasuaji mdogo na mkubwa na gharama za kulazwa,"amefafanua Konga.

Pia amesisitiza kuwa, ni matarajio ya Serikali baada ya kukamilisha mchakato huu unaoendelea na wananchi wakakata bima ya afya kwa wote wengi itasaidia mfumo kuwa imara zaidi.

"Tukiwa wengi hilo linawezekana na ikiwa wengi zaidi watajiunga hakutakuwa na ulazima wa grace period, kwa sababu mfumo wetu utakuwa imara. Changamoto iliyopo kwa sasa ni kwamba asilimia 85 ya wananchi bado hawajajiunga na bima ya afya, na asilimia 99 ya waliojiunga ni wagonjwa tayari,"amefafanua Konga.

WHO

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) chini ya Umoja wa Mataifa, Bima ya Afya kwa Wote ni fursa muhimu katika jamii ili kuhakikisha watu wote wanapata huduma za matibabu wanazohitaji bila kutatizika kifedha.

Hii inajumuisha hatua zote za msingi ikiwemo huduma bora za afya ili kuendelea kulinda nguvu kazi ya jamii na Taifa.

WHO inafafanua kuwa, bima hiyo inawezesha kila mmoja kupata huduma zinazohusiana na sababu kuu za chanzo cha maradhi na kuhakikisha kuwa ubora wa huduma hizo unafaa kuimarisha afya ya watu wanaozipokea.

Pia kuwalinda watu na athari za kulipia huduma za afya kutoka katika mifuko yao, kwani hupunguza hatari ya watu kusukumwa kuingia katika umaskini kwa sababu maradhi yasiyotarajiwa huwahitaji kutumia akiba yao, kuuza mali, au kukopa, hivyo kuharibu mustakabali wao na hata wa watoto wao.

Aidha, kufanikiwa kwa bima hiyo kwa ufanisi kunatajwa na WHO kuwa,mojawapo ya malengo yaliyowekwa na mataifa mbalimbali duniani kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu mwaka 2015.

Nchi ambazo zimepiga hatua katika bima ya afya kwa wote, zinaelezwa zitapiga hatua pia katika mambo mengine yanayohusiana na afya,kiuchumi na kijamii.

Hayo yanatokana na ukweli kwamba, afya njema huwezesha watoto kusoma na watu wazima kujipa nafasi ya kufanya kazi kwa bidii, hivyo kuzalisha mapato, husaidia watu kukwepa umaskini, na kutoa msingi wa maendeleo ya kiuchumi ya muda mrefu katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news