Rais Dkt.Mwinyi aomboleza kifo cha Mheshimiwa Benard Membe

NA DIRAMAKINI
Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kupokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyabainisha hayo Mei 12, 2023 kupitia taarifa aliyoitoa katika mitandao yake rasmi ya kijamii ikiwemo Twitter.

"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya kifo cha ndugu Benard Membe ambaye alikuwa kiongozi mwenye uwezo mkubwa, mwanadiplomasia,na mtumishi shupavu wa taifa.

"Natoa pole kwa familia, marafiki na wote walioguswa na msiba huu. Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani.Amin,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Mheshimiwa Membe amefariki Mei 12, 2023 majira ya asubuhi katika Hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es Salaam, baada ya kupelekwa kwa ajili ya matibabu. Msaidizi wa Membe, Allan Kiluvya alieleza kwa vyombo vya habari kuwa, Mheshimiwa Membe alipata changamoto ya kifua.

Membe ni nani?

Aidha, Mheshimiwa Membe amefariki akiwa na miaka 69 kwani alizaliwa Novemba 9, 1953 huko Rondo, Chiponda mkoani Lindi, wakati huo Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania ikiwa chini ya himaya ya mkoloni, Mwingereza.

Alianza kupata elimu yake ya msingi mwaka 1962, katika shule ya Chiponda, Lindi. Elimu ya sekondari aliipata shule ya Namupa Seminary, Lindi. Sekondari kidato cha tano na sita aliipata Itaga Seminary, Tabota.

Membe alisoma sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nchini Tanzania. Alijiendeleza kielimu, katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, nchini Marekani katika fani ya Uhusiano wa Kimataifa kati ya mwaka 1990 na 1992.

Baada ya kumaliza masomo ya juu nchini Marekani mwaka 1992, Membe alipewa kazi ya kuwa mshauri katika Ubalozi wa Tanzania, huko Ottawa nchini Canada, kutoka mwaka huo hadi 2000.

Membe alikuwa mwanachama mkogwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kukitumia chama hicho katika nafasi ya Ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwongo mmoja na nusu kutoka mwaka 2000 hadi 2015.

Kufuatia uchaguzi mkuu wa 2005, uliomuweka madarakani Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,Membe aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ya Oktoba 2006, yakamuhamisha na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini.

Chini ya Serikali hiyo hiyo, Membe akashika nyadhifa kubwa zaidi, pale alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akichukua kijiti hicho kutoka kwa Asha-Rose Migiro. Alikaa katika nafasi hiyo kutoka 2007 hadi 2015.

Membe alipata kushika wadhifa wa uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Umoja wa Afrika, mwaka 2008. Pia, alikuwa mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe mwaka 2013 kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Tanzania ilifungua balozi katika nchi mbalimbali duniani. Pia, Tanzania ilipokea viongozi wakubwa ulimwenguni kama Rais wastaafu wa Marekani George W. Bush, Barack Obama, Xi Jinping (China) na Jacob Zuma (Afrika Kusini).

Mbio za urais

Aidha, Membe alikuwa miongoni mwa makada wa CCM alioingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya chama hicho kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Jina lake likawa miongoni mwa yaliyokatwa na kupitishwa jina la hayati Dkt.John Pombe Magufuli.

Februari 2020 alifukuzwa uanachama na CCM, kupitia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, akituhumiwa kukiuka miiko na katiba ya chama. Mwenyewe alikana tuhuma hizo na kusema alifukuzwa kwa kuwa alitaka kugombea na kushindana na Magufuli ili ateuliwe kuiwakilisha CCM katika ngazi ya urais.

Membe alijiunga na ACT Wazalendo Julai 2020, na kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huo, na kupata asilimia 0.5 ya kura zote. Uchaguzi ambao ulimrudisha Magufuli wa CCM madarakani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news