Rais Dkt.Samia ataka vikwazo mpakani viondolewe

LILONGWE-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara hususani mpakani mwa Tanzania na Malawi ili wananchi waweze kunufaika na biashara zao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa na mwenyeji wake Rais wa Malawi, Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wakati wakishuhudia utiaji Saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Malawi kuhusiana na ushirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mara baada ya mazungumzo yao Lilongwe nchini Malawi Julai 7, 2023. Aliyeketi (kulia) ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape Moses Nnauye wakisaini mkataba huo pamoja na Waziri wa Habari na TEHAMA wa Malawi, Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa wa kwanza (kushoto). (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Julai 6, 2023 kabla ya kuhitimisha ziara yake ya Kiserikali ya siku tatu nchini Malawi, ambapo pia amehudhuria sherehe za miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo.

Kwa pamoja, Rais Dkt.Samia na Rais wa Malawi, Dkt.Lazarus McCarthy Chakwera wamewataka mawaziri husika kukaa chini na kutafakari namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara ili maono ya Serikali zote mbili yaweze kufikiwa.

Rais Dkt.Samia pia alishuhudia utiaji saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Malawi kuhusiana na mashirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Katika mkataba huo, upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye pamoja na Waziri wa Habari na TEHAMA wa Malawi, Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashwa.

Vile vile Rais Dkt.Samia ameipongeza Malawi kwa kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika shule zake na kusisitiza kwamba lugha hiyo ndio itakayowaunganisha Waafrika.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Samia alitembelea eneo la Kapeni view point Blantyre na kujionea athari zilizotokana na kimbunga Freddy ambapo watu wengi walipoteza maisha, mali na makazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news