Uchumi thabiti wa Zanzibar

NA GODFREY NNKO
 
RIPOTI ya Uthabiti wa Kifedha Tanzania Disemba 2022 imeonesha kuwa, uchumi wa Zanzibar uliendelea kuwa imara kufuatia kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi ambazo ziliathiriwa na janga la virusi vya UVIKO-19.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba na Gavana mstaafu wa BoT, Prof. Florens Luoga na Uongozi wa BoT, Januari 18,2023 wakiwa katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar, alipofika na uongozi wake kwa mazungumzo na kujitambulisha.(File/Ikulu).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kila mwaka ambayo huwa inatolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwa imetayarishwa na benki hiyo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha nchini imeainisha kuwa,ukuaji wa uchumi wa Zanzibar mwaka 2022 ulikadiriwa kuwa asilimia 5.9.

Mafanikio hayo yanatajwa kuchochewa na ongezeko la shughuli za kitalii visiwani humo ukiwemo uwekezaji katika sekta mbalimbali za umma na binafsi.

Aidha, ukuaji huo unaungwa mkono na Serikali kupitia juhudi za kuimarisha mfumo wa usimamizi wa kodi, walipakodi kufuata sheria zilizopo na mifumo ya udhibiti, na uwekaji kidijitali wa huduma za uwekezaji.

Pia, juhudi za Serikali kutumia uwezo wa uchumi wa buluu katika matumizi endelevu ya rasilimali za baharini umetajwa kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kusaidia uchumi wa Zanzibar kuendelea kustawi.

Ripoti hiyo imetaja kuwa,uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.1 mwaka 2023 kutokana na dhamira thabiti ya Serikali ya kuweka mazingira mazuri ya biashara, uthabiti wa kisiasa, na mifumo mizuri ya kukabiliana na athari zilizochangiwa na janga kubwa la UVIKO-19.

Mbali na hayo, ripoti hiyo imebainisha kuwa, mfumuko wa bei ulibaki kuwa juu mwaka huo kutokana na kuongezeka kwa bei za vyakula na nishati, licha ya utulivu na sera nzuri za usimamizi wa fedha.

Desemba 2022,mfumuko wa bei ulipanda hadi asilimia 8.1 kutoka asilimia 2.4 iliyorekodiwa mwaka uliopita, juu kidogo ya vigezo vya muunganiko wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) visivyozidi asilimia 8.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kuongezeka huko kulichangiwa zaidi na bei ya juu ya vyakula, hasa unga wa mahindi, mchele na unga wa ngano, na bei ya mafuta pamoja na kukatika kwa minyororo ya ugavi katika soko la Kimataifa.

Aidha, ripoti hiyo inabainisha kuwa, juhudi endelevu za ndani kupitia usimamuzi wa mwenendo wa sera ya fedha unatarajiwa kudumisha mfumuko wa bei ndani ya kikomo kimoja.
Bofya hapa, kupakua ripoti yote
 
BoT ni mshauri mzuri

Januari 18, 2023 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni mdau muhimu wa sekta ya maendeleo Zanzibar na ni mshauri mzuri kwa masuala ya uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na Gavana mpya wa benki hiyo, Emmanuel Mpawe Tutuba, aliyefika kujitambulisha tangu alipoteuliwa Januari 7, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua na ushirikiano mzuri na BoT wakati wote pamoja na kupata ushauri mzuri wa uendeshaji wa uchumi wa Zanzibar.

Pia aliongeza kuwa, Zanzibar imepata mafanikio makubwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania na kueleza ushirikiano wa taasisi mbili hizo umejenga ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao ipasavyo.

Rais Dkt.Mwinyi alimuahidi Gavana huyo kushirikiana naye kwenye majukumu yake kwa kipindi chote cha uongozi wake na kumshauri kuendeleza alipofikia mtangulizi wake.

“Nikupe ahadi tu ya ushirikiano wetu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tukiwa wadau muhimu wa kazi zinazofanywa na Benki Kuu, tupo tayari kushirikiana vya kutosha kwa masuala yote yanayohitaji ushirikiano wetu,” aliahidi Rais Dkt.Mwinyi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alimuahidi Gavana huyo kufanya naye kazi bega kwa bega kwa msaada mkubwa wa Wizara ya Fedha na Mipango (Wizara ya Fedha) pamoja na taasisi zake, na kuongeza kwamba kazi nzuri ambayo ilifanywa na mtangulizi wake, Prof.Florens Luoga ilileta mafanikio makubwa kwa Serikali.

Akizungumzia changamoto za uchumi wa Dunia,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alimweleza Gavana Tutuba kwamba washirikiane kutafuta ufumbuzi mzuri wa kuzigeuza changamoto hizo kuwa fursa ili zilete tija kwa taifa pamoja na kuziangalia kwa kuzidhibiti ili zisiathiri uchumi wa nchi.

Rais Dkt.Mwinyi alimuahidi Gavana huyo kushirikiana naye kwenye majukumu yake kwa kipindi chote cha uongozi wake na kumshauri kuendeleza alipofikia mtangulizi wake.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alimshuru Gavana aliyemaliza muda wake, Prof. Florens Luoga kwa ushirikiano wake alioutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi chote cha utumishi wake kwa Taifa, na kueleza kwamba wakati mwingine hakuishia tu kwenye ngazi ya wizara bali alifika hadi ngazi za juu katika kufanikisha majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu.

Naye Gavana Tutuba alisema, Benki Kuu ya Tanzania ni chombo cha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kinachofanya kazi zake kwa pande zote mbili za Muungano katika kusimamia masuala ya kiuchumi na sera za fedha kwa Zanzibar na Bara.

Alisema,Serikali zote mbili zipo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi kwa kudhibiti mfumuko wa bei duniani uliochangiwa na athari kubwa za kupanda kwa bei za mafuta ambayo inaathiri zaidi sekta ya usafirishaji kwa wananchi.

Gavana Tutuba alitumia fursa hiyo kuzipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wake kuwapunguzia makali yanayotokana na athari hizo.

Naye Gavana wa zamani, Prof. Florens Luoga alitumia fursa hiyo kumuaga Rais Dkt.Mwinyi baada ya kumaliza muda wa utumishi wake kwa Benki Kuu ya Tanzania pia aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano iliyoutoa kwake muda wote wa utumishi wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news