NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM) kwa kuuza Dola za Marekani milioni 15.75 kupitia mnada wa ushindani, hatua inayolenga kuimarisha ukwasi na kuleta utulivu katika soko la fedha za kigeni nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya BoT, ushiriki huo umefanyika kwa kuzingatia Sera yake ya ushiriki katika Soko la Fedha za Kigeni ya mwaka 2023.Aidha,katika mnada huo, kiwango cha wastani cha kubadilisha fedha kilichokubaliwa kilikuwa Shilingi 2,572.56 kwa Dola moja ya Marekani.
Pia,taarifa hiyo imeeleza kuwa, jumla ya Dola za Marekani milioni 15 zilitangazwa kwa ajili ya mnada huo, huku kiasi kilichowasilishwa na washiriki kikifikia Dola milioni 27, hali inayoonesha mwitikio mkubwa wa taasisi za fedha. Kati ya kiasi hicho, Benki Kuu ilikubali zabuni zenye thamani ya Dola milioni 15.75.
Kwa mujibu wa matokeo ya mnada huo, viwango vya juu na vya chini vya ushindani vilikuwa Shilingi 2,580.00 na Shilingi 2,560.00 kwa Dola moja ya Marekani mtawalia.
Aidha, viwango vya juu na vya chini vilivyokubaliwa vilikuwa Shilingi 2,580.00 na Shilingi 2,570.00 kwa Dola moja ya Marekani.
Vilevile,jumla ya benki 30 zilishiriki katika mnada huo, ambapo benki 18 zilifanikiwa kushinda zabuni zao.
