KIGOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara kutoka Kanda ya Magharibi, kwa lengo la kuongeza uelewa na umahiri wao katika kuripoti kwa usahihi masuala yanayohusu shughuli na majukumu ya Benki Kuu.
Mafunzo hayo yamefanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 26 hadi 27 Februari 2026 na kuwashirikisha jumla ya waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Kagera.Akisoma hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Meneja wa Mawasiliano wa BoT, Bi. Victoria Msina, Meneja Msaidizi wa Uhusiano wa Umma, Bi. Noves Moses, alisema kuwa,semina hizo zinalenga kuimarisha ubora na usahihi wa uripotiji wa habari zinazohusu Benki Kuu na mchango wake katika uchumi wa taifa.
Aidha, Bi. Noves alibainisha kuwa mwaka huu BoT inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, na kwamba maadhimisho hayo ni fursa kwa waandishi wa habari kuandika makala zinazoangazia mchango wa Benki Kuu katika ukuaji wa uchumi pamoja na kuenzi kazi inayofanywa na BoT katika kusimamia uthabiti wa uchumi wa nchi.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni: Majukumu ya Benki Kuu na utekelezaji wa Sera ya Fedha ikiwemo Riba ya Benki Kuu; umuhimu wa ununuzi wa dhahabu na faida zake katika kuimarisha akiba ya taifa; usimamizi wa mifumo ya malipo ya taifa; utambuzi wa alama za usalama katika noti; pamoja na namna BoT inavyopokea na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha.





